Friday, 26 September 2014
JK AAHIDI SHERIA YA HABARI FEBRUARI 2015
TANZANIA inatarajiwa kupata Sheria ya Uhuru wa kupata Habari ifikapo Februari, mwakani. Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana alipokuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano unaohusu Uwazi na Ushirikiano kati ya Serikali na Jamii.
Rais Kikwete alisema rasimu ya muswada wa Uhuru wa kupata Habari uko katika hatua ya mwisho ambapo wadau mbalimbali wanashauriana na kutoa maoni tayari kupelekwa bungeni.
Oktoba mwaka jana, katika mkutano wa Open Government Partnership (OGP) jijini London, Rais Kikwete alitangaza nia na ujasiri ulioko serikalini kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na sheria ya uhuru wa habari.
Alisema uhuru wa habari ni muhimu kwa wananchi kwa sababu: "Ni haki yao ya msingi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu maisha yao," na kuongeza: "Ni muhimu wananchi kujua serikali yao inafanya nini kwa niaba yao".
Akizungumza katika mkutano huo jana, Rais Barack Obama wa Marekani alisema OGP ni ubia kati ya Serikali na wananchi wake. Viongozi wengine waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na wa Indonesia, Afrika Kusini na Ufaransa.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa UN kuhusu elimu ambaye amemshukuru na kumsifu Rais Kikwete kwa kusimamia elimu nchini.
Wabia hao ni pamoja na Shirika la Global Education, Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wawakilishi wa Serikali ya Uingereza na Benki ya Dunia.
Wengine ni kutoka Global Business Coalition na Dubai CARES ambao kwa pamoja wanataka kuinua kiwango cha Elimu ya Msingi na Sekondari kwa kusaidia na kuchangia ili kuboresha zaidi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment