TAASISI ya HakiArdhi imesema kuwa mfumo wa ardhi nchini unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wanasiasa kuingilia utendaji na maamuzi yaliyofanywa na wataalam kwa ajili ya kulinda maslai yao ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji Yefred Myenzi alisema kuwa kutokana na changamoto mbalimbali zinazoukabili mfumo huo wameamua kutumia maadhimisho ya miaka 20 ya taasisi hiyo ili kutafakari kwa kina changamoto hizo na kuzitafutia suluhu ya kudumu.
Myenzi alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kutathmini na kutafakari juu ya mabadiliko katika mfumo huo na kuweka mikakati ya pamoja ili kuhakikisha mfumo wa milki ya ardhi unamlinda mzalishaji mdogo.
Alisema kuwa kongamano hilo la siku mbili litakutanisha washiriki 150 kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwemo na wa nje ya nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe.
Alisema kuwa dhima kuu ya kongamano hilo ni ‘mabadiliko katika mfumo wa milki ya ardhi na hatma ya wazalishaji wadogowadogo; Tathmini ya miaka 20 ya harakati’.
“Lengo la kongamano ni kutoa fursa kwa wananchi (washiriki) ili watoe dukuduku zao kuhusiana na matatizo ya ardhi wanayokumbana nayo katika maeneo yao pamoja na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa milki ya ardhi nchini,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazoukabili mfumo huo ni kukithiri kwa migogoro ya ardhi baina ya makundi mbalimbali ya watumiaji, Ukiukwaji mkubwa wa sheria za ardhi katika ugawaji, usimamizi na matumizi ya ardhi.
Akitolea mfano baadhi ya wawekezaji katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Manyara wamebadili matumizi ya ardhi bila kufuata utaratibu na hakuna hatua walizochukuliwa.
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment