. Ajira ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba Zdravko Logarusic imefikia tamati rasmi jana baada ya uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba wake.
Logarusic, maarufu kwa jina la Loga alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha Simba mwezi uliopita, ikiwa ni hatua ya kuongeza ule wa miezi sita ambao aliusaini Desemba mwaka jana wakati akichukua nafasi ya wazawa Abdallah Kibaden ‘King’ na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Akitangaza uamuzi huo katika mkutano mfupi uliotumia dakika tano tu kwenye Hoteli ya Serena, Rais wa Simba, Evans Aveva alisema wamelazimika kusitisha mkataba na Loga kwa sababu ya hulka na tabia ya mwenendo wa kocha huyo kushindwa kuendana na ule wa Simba.
Aveva alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, uongozi wake ulikuwa na vikao vingi na Loga vikimtaka kubadilika kila anapokuwa anaonyesha toafuti, lakini ilishindikana.
“Kutokana na hilo leo (jana) asubuhi, niliitisha kikao cha Kamati ya Utendaji kujadili tatizo hilo na tukakubaliana kufanya uamuzi huo, lengo likiwa kuinusuru klabu yetu,” alisema Aveva.
“Tulikutana na kocha mwenyewe baada ya mimi na kamati yangu kuona tuchukue uamuzi huo na hata yeye mwenyewe alikubaliana na hilo kwamba ni vyema tukaachana kwa hali ya amani.
“Niwahakikishie Wanasimba kuwa uamuzi huu tumeuchukua baada ya kufanya tafakuri ya kina na haya yote tunayafanya ikiwa ni kuzidi kubeba dhamana, ambayo wametupa mimi na kamati yangu ya utendaji kwa ajili ya mafanikio ya klabu yetu ya Simba na tunamshukuru na kumtakia kila la kheri kocha Logarusic.
Juzi baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Simba na Zesco ambao Wekundu hao walilala kwa mabao 3-0, ilibainika kuwa Loga alikuwa mkali kwa baadhi ya wachezaji wake na kuwatolea lugha kali, huku akitangaza kwamba baadhi yao hataki kuingia nao kambini.
“Ni kweli nilikuwa mkali kwa baadhi ya wachezaji baada ya mchezo, mimi ni kocha na Simba ilinikabidhi jukumu la kuongoza timu, huku uongozi ukiangalia utawala, siwezi kuwa na furaha na mchezaji ambaye hataki kufuata kutekeleza,”alisema Loga saa chache kabla ya kufutwa kazi.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kimeliambia gazeti hili kuwa, Loga ametimuliwa kutokana na kitendo cha kuwatukana wachezaji akiwatuhumu kuonyesha kiwango duni wakati wa mechi dhidi ya Zesco.
“Ebu fikiria ilifikia hatua ya kuwaambia wachezaji waliokuwa timu ya taifa kwamba hawana msaada, aliwambia Kiemba (Amri) na Uhuru (Selemani) watafute timu ya kwenda kwa mkopo hataki kuwaona, huyu kocha anafaa kweli,” kilieleza chanzo hicho.
“Tulimvumilia sana kwa sababu wachezaji walikuwa wanalalamika kutukanwa na wakati mwingine kwa jambo dogo la kumwelekeza mchezaji, hakufanya hivyo zaidi ya kufoka.”
Kufuatia kuondoka kwa Loga, taarifa za kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa tayari Wekundu hao wameanza mazungumzo na Kocha Mzambia, Patrick Phiri ambaye ndiye anapewa nafasi kubwa ya kuchukua timu.
2 comments:
Alhaji Chambo16:27
1
Reply
yaah ujue uongoz ndo mbofu sio kocha ndo ivyo 2 magol yamewachanganya....
Alhaji Chambo16:27
1
Reply
yaah ujue uongoz ndo mbofu sio kocha ndo ivyo 2 magol yamewachanganya....
Post a Comment