KIKONGWE Athumani Kulaba (80) mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, amewashangaza wakazi wa eneo hilo alipobainika kuwa anakula udongo kama chakula kwa zaidi ya miaka 10.
Kwa mujibu wa kikongwe huyo aliyezungumza kwa shida, alisema kwa sasa amezoea hali hiyo, licha ya kupewa chakula kutoka kwa wasamaria wanaofika nyumbani kwake.
Alisema sababu ya kula udongo ni ugumu wa maisha alionao hasa baada ya kutelekezwa na aliyekuwa mwajiri wake na kutomlipa fedha zake.
“Hili eneo sio langu, niliachiwa nilinde na tajiri yangu ninayemfahamu kwa jina moja la Musada karibu miaka 20 iliyopita ambapo awali alikuwa akinilipa lakini ghafla alisitisha malipo hadi sasa,” alisema kikongwe huyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Chanika, Mohamed Katungi alikiri kupokea taarifa hizo kutoka kwa jirani wa Kulaba.
Alisema baada ya jirani huyo kuona hali ya mzee inazidi kuwa mbaya, alimtaarifu mjumbe wa eneo hilo John Kanguya ili kumpeleka kituo cha afya Chanika ambapo aligundulika kuwa na Safura.
“Uwezekano wa kikongwe huyo kuishi kwa kula udongo inawezekana kwa sababu nyumba yake imemeguka pia ukizingatia eneo zima wanaishi watu wawili tu, kitu kilichosababisha watu wasijue maisha yao,” alisema Katungi.
Aliwaomba watanzania wamsaidie kwa kuwa anahitaji nauli ya kurudi kwao Bukene, Tabora. Kwa atakayeguswa awasiliane na mwenyekiti wa mtaa huo kwa namba 0784 295 833 au 0715 295 833
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment