Tuesday, 1 July 2014

WANAOKATAA KADI ZA NHIF KUKIONA"


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF ) kutoa taarifa za watumishi wa vituo vya afya wanaowadhalilisha wagonjwa kwa kigezo cha matumizi ya kadi, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Aidha, ameziagiza halmashauri za manispaa za Jiji la Dar es Salaam kuharakisha mchakato wa uchukuaji wa maoni kutoka kwa wananchi kwa ajili ya uanzishwaji wa utaratibu wa huduma kwa kadi (TIKA) ili kuwapunguzia usumbufu usio wa lazima wakati wa matibabu.
Sadik aliyasema hayo Dar es Salaam jana kupitia hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi wakati wa ufunguzi wa mkutano ulioandaliwa na NHIF kwa wadau wa mfuko huo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini, taasisi, wabunge, wakuu wa wilaya na wengineo.
Alisema wakati huu ambapo matumizi ya kadi kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali yanaendelea kushika kasi ulimwenguni kote, kumekuwa na dhana potofu miongoni ya baadhi ya watoa huduma kuthamini wagonjwa wanaotoa fedha taslimu na kuwadharau wale wanaotumia kadi za bima ya afya.
“Ni lazima tabia hii ikome mara moja na ni lazima mtambue kwamba mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya na kupunguza utaratibu wa wagonjwa kutoa fedha taslimu kwa namna moja au nyingine.”
“Kupitia mkutano huu, ninatoa rai kwa wanachama wa mfuko kutoa taarifa mara wanapobaini uwepo wa udhalilishaji katika vituo vya huduma ili mtumishi yeyote atakayebainika kumdhalilisha mgonjwa kwa kigezo cha kutumia kadi ya bima ya afya aweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Sadick.
Aidha, kuhusu kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa utaratibu wa tiba kwa kadi kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na kasi isiyoridhisha, Sadik alisema ni sawa kutowatendea haki wananchi ikizingatia kwamba lengo la Serikali ni kufikia asilimia 30 ya Watanzania kuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2015.
“Kwa maana hiyo ninatoa rai kwa manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo bado hazijakamilisha ukusanyaji wa maoni kwa wananchi kukamilisha mara moja ili tuweze kufikia lengo lililowekwa na Serikali,” alisisitiza.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bima ya Afya, Balozi Ali Mchumo aliwataka waajiri wote kuhakikisha wanawasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati ili kuepusha usumbufu usio wa lazima huku akielezea nia ya NHIF kuandaa utaratibu wa kuwashughulikia waajiri wanaochelewesha michango hiyo ili iwe fundisho kwa wengine

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!