Rio de Janeiro, Brazil. Ujerumani na Argentina kila moja inashuka kwenye Uwanja wa Maracana kwa lengo moja tu la kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.
Ujerumani wanasaka taji la nne tangu walipofanya hivyo mwaka 1990 kwa kuinyuka Argentina 1-0, wakati Argentina wenyewe wana ndoto ya kunyakua ubingwa wa tatu tangu walipotwaa taji hilo 1986 kwa kuifunga Ujerumani 3-2.
Hata hivyo, Ujerumani wanaingia uwanjani wakiwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya Argentina baada ya kuiondoa mara mbili kwenye nusu fainali 2006 kwa penalti na 2010 katika robo fainali wakiichakaza kwa mabao 4-0 nchini Afrika Kusini.
Meneja wa timu ya Ujerumani, Oliver Bierhoff alisema wamewatahadharisha wachezaji wake kuwa watulivu kama presha itakuwa kubwa Maracana.
“Waargentina ni watu wazuri na ni timu nzuri tunayokutana nayo, lakini kiwanja kitakuwa na mabadiliko makubwa kwa mchezaji mmoja, mmoja hivyo tunatakiwa kuwa tayari,” alisema Bierhoff.
Bierhoff alisema Ujerumani inajiandaa kupata ushindani mkali kuliko ilivyokuwa waliposhinda 7-1 dhidi ya Brazil katika nusu fainali.
“Wanajilinda zaidi, na kutengeneza nafasi kidogo za Lionel Messi kuonyesha uwezo wake,” alisema Bierhoff. “Tunatakiwa kucheza mchezo wetu, kukimbia zaidi na kutowapa nafasi ya kutosha ya kucheza wanavyotaka.”
Tayari Fifa imeshamtangaza Mtaliano Nicola Rizzoli kuchezesha mechi hiyo ya fainali leo.
Argentina wamekuwa wakifanya mazoezi bila ya kuruhusu mashabiki kutazama wakati wakijiandaa na mechi hiyo.
Zaidi ya mashabiki 100,000 wa Argentina wanatarajiwa kuwepo kwenye Uwanja wa Maracana kushuhudia mechi hiyo.
Ulinzi mkali Maracana
No comments:
Post a Comment