Hatimaye Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwania urais amethibitisha rasmi kuwa atagombea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Kiongozi huyo aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu wakati alipokuwa akihojiwa na Radio Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani jana mchana na hivyo kuwa kiongozi wa pili kutangaza nia kupitia vyombo vya habari vya kimataifa.
Julai 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba alitangaza nia ya kuwania urais baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) alipokuwa amekwenda huko kuhudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano.
Akifafanua kwa nini anataka kuwa rais, January alisema kuwa huu ni wakati wa fikra mpya kushika dola na kwamba anaamini muda wa wazee kukaa kando umefika.
Sumaye ambaye aliwahi kugusia suala hilo kwa kusema kuwa angeweza kugombea kwenye kinyang’anyiro kijacho kama wananchi wangetaka afanye hivyo sasa ametegua kitendawili kwa kusema kuwa yuko tayari kuwania nafasi hiyo.
“Maana siyo kila mtu anayejaza kutaka kwenda kugombea. Ni watu wamemtaka na wapo wengi tu ambao wanajaza kwa sababu wametaka wenyewe eeh! Kwa hiyo kama watu wakinitaka nitagombea kwa nini nisigombee, nitagombea na ninafikiria nitagombea,” alisema.
Hata hivyo, alionyesha kutishwa na kiwango cha rushwa katika mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kusema kuwa:
“Ukweli ni kwamba matumizi ya fedha ndiyo yamekuwa makubwa sana na kwa kiwango fulani Watanzania wanadhani, siwezi kuwamo. Watanzania ni wale ambao wana nafasi ya kuchagua na wanadhani kama hawajapata fedha basi huyo ambaye hajatoa fedha anaonekana kama hachaguliki.
“Ukweli ni kwamba ni jambo la hatari na lazima tulipige vita katika nchi yetu. Matumaini yangu ni kwamba viongozi wetu waliopo watajitahidi kupiga vita,” alisema Sumaye.
Pia kiongozi huyo alikosa baadhi ya watu wanaosema wakati wa kuwa na rais kijana umefika kwa kusema kuwa umri hauwezi kuwa kigezo pekee cha kumpata rais.
“Kama kuna kijana hata kama ana miaka 41 ambaye anadhani anafaa na umma unadhani anafaa si kwa sababu ni kijana hakuna tatizo, mradi asiwe anakwenda pale kwa kusema mimi ni kijana ninayefaa. Unaweza kusema kila kijana anafaa kuongoza hii nchi? Haiwezekani” alihoji.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa Januari 1 mwaka huu alitangaza ‘kiaina’ kuwania nafasi ya urais kwa kusema kwamba anaanza safari ya matumaini.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment