Monday, 7 July 2014

UHAMIAJI KUBADILI TENA HATI ZA KUSAFIRIA

Mathias Chikawe
Idara ya Uhamiaji nchini imesema inatarajia kubadili pasipoti za kusafiria kutokana na kuwapo kwa matumizi mabovu kwa baadhi ya wananchi. 

Akizungumza kwenye banda la Uhamiaji katika viwanja vya maonyesho ya 38 ya kimataifa ya biashara  ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano wa idara hiyo,  Tatu Buruhani, alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na changamoto kubwa iliyopo kwa wananchi ya kuwa na hali ya udanganyifu katika uwasilishaji wa vitu ambavyo vinahitaji kupata hati hizo za kusafiria. 
Alisema, wananchi wengi wamekuwa wakiwatumia mawakala maarufu kama vishoka  wa idara hiyo kwa nia ya kupatiwa huduma hiyo  kwa haraka na hivyo kuwasababishia  wengi wao   kutapeliwa ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa vyeti vyao.
 
“Kinachotokea hapa ni kwamba, mwingine anachukua ile pasipoti anakwenda kuweka rehani, mwingine anauza, halafu anakuja kukwambia kwamba ameibiwa. Katika uchunguzi tuliofanya tumebaini  kuwa hawaibiwi bali wanazitumia vibaya pasipo kutambua umuhimu wake,” alisema Buruhani na kuongeza:
 
“Wengine wanapotaka pasipoti hawafiki huku, wanaishia kwa wale mawakala wetu, wanadanganywa kule, kule mtu anamwambia nipe labda laki tatu, nitakutafutia utapata, kitu ambacho hana uwezo nacho.
 
Matokeo yake wanakuja kulalamika kuwa wameibiwa, na hii ni kutokana na watu kutaka mambo ya haraka, na imani walizo nazo kuwa wakija huku ni lazima watoe rushwa, hiyo  kwetu haipo.”
 
Kwa mujibu wa Buruhani, utaratibu wa kubadilisha huduma ya hati za kusafiria  ulianza  mwaka 1961 kutokana na changamoto hizo na kwamba walifanya mabadiliko mengine katika miaka ya  1992 na 2005 na kwamba matarajio mengine ya kufanya hivyo ni  mwaka huu.
 
SOURCE: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!