MABADILIKO ya tabia nchi na kukithiri kwa matumizi ya vyakula vinavyozalishwa kwenye viwanda mbalimbali ndani na nje ya nchi, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa magonjwa mbalimbali ya binadamu na wanyama.
Matibabu ya magonjwa hayo mara nyingi yamekuwa ni ghali jambo linalofanya uchumi wa nchi, mgonjwa au familia inayouguza kushindwa kumudu au kulazimika kutumia nguvu za ziada hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi kusuasua.
Matatizo ya figo ni miongoni mwa magonjwa yanayoonekana kuwapata watu wengi hapa nchini.
Mara kwa mara kumekuwa na taarifa za figo moja au mbili kugoma kufanya kazi au kuharibika kutokana na sababu mbalimbali.
Dk. Mohamed Mkweli wa kituo cha tiba mbadala cha Afya Bora kilichopo, Kigogo jijini Dar es Salaam, anaeleza changamoto, tiba na sababu za kushamiri kwake licha ya kuongezeka kwa utaalamu na vituo vya kutolea matibabu vyenye vifaa vya kisasa zinavyoendana na teknolojia.
Anasema ugonjwa wa kuharibika kwa figo hautibiki kirahisi pamoja na kuwa wataalamu wa afya wanasema zipo sababu kadhaa zinazochangia kuongezeka kwake ikiwemo matumizi mabaya ya dawa, hasa za maumivu zinazotumiwa kila wakati mtu anaposikia vibaya bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Dk. Mkweli anabainisha kuwa sababu nyingine ni matumizi ya sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na dawa kutoka nchini China zinazoletwa kwa njia zisizostahili bila kupitia kwenye vyombo vinavyohusika kuthibitisha ubora wake.
Anasema kuharibika kwa figo ambayo ina kazi ya kuchuja uchafu uingiao kwenye mwili hufanya viungo vingine vya mwili viathirike na hivyo mgonjwa hujisikia vibaya zaidi na kuhitaji matibabu makubwa yanayogharimu fedha nyingi iwe ndani au nje ya nchi.
Anabainisha kuwa kituo chake kimefanikiwa kutibu ugonjwa huo ikiwemo hata tatizo la kuondoa sumu katika mwili wa binadamu ambapo husafisha figo na damu kwa kutumia dawa zilizopimwa na kuthibitishwa huku akifanya hivyo kwa gharama ambazo watu wenye kipato kidogo wanaweza kumudu.
Anasema humpa mgonjwa dawa inayotoa maji yasiyohitaji kutoka kwenye damu yake baada ya figo kushindwa kufanya kazi na taka hizo kuingia kwenye mfumo wa damu.
Anasema kwa kawaida figo hufanya kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya watu huathirika na figo zao kushindwa kufanya kazi ya kuchuja uchafu huo kutokana na sababu mbalimbali alizozitaja hapo juu.
“Figo ni miongoni mwa viungo muhimu katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu,” anasema.
Dk. Mkweli anazitaja kazi kuu za figo kuwa ni kuchuja sumu katika damu, kusaidia kuhifadhi, kudhibiti kiwango cha maji na madini mwilini.
Anaeleza kuwa figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.
Anaeleza kuwa kazi nyingine za figo ni pamoja na kusaidia kutengeneza kiasili cha erythropoletin ambacho ni muhimu katika utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu, hupokea asilimia 25 ya damu na kila figo ina chembechembe hai ndogo milioni moja, pia kusaidia kudhibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini.
VIA -TZ DAIMA
No comments:
Post a Comment