Pages

Monday, 21 July 2014

NASEMA HIVI! WAACHENI WAULILIE URAIS 2015 WATANYAMAZA!

MTOTO akililia wembe mpe, ukimkata atauacha. Hakuna ambaye amefika hapo alipo bila kukumbwa na mikasa au misukosuko ya hatari wakati akiwa mtoto kwa lengo la kuutafuta ukubwa kwa nguvu na haraka.

Hali hiyo haitofautiani sana na mawazo ya wanasiasa. Kila mwanasiasa amejiwekea mipango na malengo yake ya kufikia mahali anapotaka, wapo wanaojiona watoto kisiasa, wapo wanaojiona vijana kisiasa na wapo waliozeeka na bado hawaachi siasa.
Kwa mazingira hayo, siasa ni ugonjwa unaoambukiza haraka fikra za mtu bila kujali rika alilonalo. Ni ugonjwa wa hatari kwa kuwa kila aliyeingia kwenye siasa hujiona ana uwezo mkubwa kuliko wenzake waliomtangulia au aliowatangulia.
Siasa kwa kiasi kikubwa inachangia kudumaza taaluma za watu waliosoma vizuri. Wanakuwa wamejikita na kubobea kwenye taaluma zao, lakini wanapoingia kwenye siasa wanagawanyika katika makundi ya watoto, vijana na wazee.
Kwa kuwa kila mmoja anaweza kupimwa kwa weledi wake na namna alivyoweza kuingia kwenye siasa, kuna kundi la watu wachache sana ambao hufanikiwa kuijua siasa kuliko kundi kubwa ambalo husindikiza wenzao bila kujua mbele waendako.
Hiyo ndiyo siasa ninayoiona mara kadhaa ikitumiwa na wajanja wachache wanaojua kile wanachokifanya kuliko kundi la watu wengi wanaoishia kuwa mashabiki na hawasomi alama za nyakati.
Kinachowatatiza Watanzania wengi ni kuacha kufanya mambo ya msingi, yanayopasa kulisukuma mbele taifa letu, tunabaki kuwasikiliza wanasiasa bila kujua werevu na wajinga walipo.
Tunaacha kujikita kule taifa linakopaswa lielekee kimaendeleo na badala yake tunapoteza muda mwingi kwenye midahalo na mijadala ya wanasiasa, hasa wanaoulilia urais usiku na mchana.
Ndiyo maana nasema hivi, ndugu zangu Watanzania waacheni wanaoulilia urais waendelee kulia, watanyamaza wenyewe, kwanini tuwafumbe midomo wakati wana kiu ya kuuzungumzia na baadae kuuwania?
Waacheni waseme, waimbe, wacheze ngoma, waende kwa waganga wa kienyeji, waunde mitandao yao, watumie fedha zao na mali zao kwa ajili ya urais, waacheni waulilie.
Kama urais unaliliwa na watoto, vijana na wazee waacheni. Kila kundi liachwe lililie urais mwisho wake wapo watakaonyamaza wenyewe.
Ikumbukwe kuwa urais ni kofia moja, hauvaliwi na vichwa viwili au vitatu, wote walioamua kuulilia wanafahamu kuwa siku ikifika atakayeweza kuupata ni mmoja tu.
Sasa kwanini watu washindwe kufanya kazi zao za msingi, tuache kupanga mipango ya kujinusuru na umasikini, tunabaki kuwazungumzia watu ambao hawana faida, wanaendelea kuwaumiza vichwa wenzao walioamua kunyamaza kimya.
Hivi kwani sifa ya urais ni kuanza kuulilia kwa gharama yoyote, au wale wanaoutaka wakiamua kunyamaza bila kupiga kelele hawawezi kuupata?
Hivi ni wangapi wanaokumbuka kuwa ‘chema chajiuza na kibaya chajitembeza’ hawaamini kuwa rais bora atapatikana kwa busara zake, hekima, uwezo, elimu na ucha mungu?
Kwanini watu wahangaike na wale wanaolilia urais kwa kujitembeza? Hawa hawaoni aibu, hawapimwi kwa busara zao, ujinga wao na hekima zao zenye upungufu mbele ya binadamu wenzao, kwanini wahangaikiwe?
Acheni waulilie, wajitembeze, wajitangaze, wapaze sauti zao kwenye vyombo vya habari ndani na nje ya nchi kuwa wao wana sifa za kuwa rais, waacheni.
Kwanini Watanzania wanaoishi katika ufukara mkubwa wanaacha kuhangaikia maisha yao wanapoteza muda mwingi kukaa vijiweni na kujadili mawazo ya mtu mmoja anayelilia urais?
Nafasi ya urais ni moja. Hata wakigombea watu 100, bado moja itabaki kuwa moja, haigawanyiki kwa mbili. Washindane ndani ya vyama vyao, washindane kwa turufu ya mgombea binafsi, lakini bado moja itabaki kuwa moja, hakuna njia mbadala ya kuigeuza nafasi ya urais kuwa kama mafungu ya nyanya sokoni.
Rais bora na anayetegemewa na Watanzania ataanza kutamkwa na wenyewe wakati ukifika, nyota yake itang’ara bila kutegemea kurunzi. Rais wa tano wa Tanzania atakuja bila kutumia kinywa chake, bali atanenewa na wanyonge kuwa huyo ndie chaguo lao.
Ni nani aliyewahi kujiuliza kuwa aliwahi kuambiwa kabla Julius Kambarage Nyerere angekuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Ni nani aliyewahi kuambiwa kuwa ‘Mzee Ruksa’ Ali Hassan Mwinyi angekuwa rais wa awamu ya pili ya Tanzania?
Nani aliyeambiwa kuwa Benjamin William Mkapa angekuwa rais wa awamu ya tatu na ikawa hivyo? Nani aliwahi kuambiwa hivyo na ni lini Mkapa  alionekana akizunguka nchi nzima akiulilia urais kabla ya wakati?
Kama hali iko hivyo ni nani aliyewahi kutabiri kwa akili zake kuwa ipo siku Jakaya Kikwete angekuwa rais wa awamu ya nne wa Tanzania. Najua hakuna aliyeshiriki kujua kiongozi yupi atatokea wapi na kwa wakati upi.
Ukweli huo unabainisha wazi kuwa rais ajaye wa awamu ya tano wa Tanzania atapatikana kwa njia ambayo Watanzania wengi hawawezi kujua, hivyo mambo ya urais yasipumbaze akili za watu makini, waachiwe wajinga wapoteze muda.
Inawezekana wapo wanaotegemea zaidi miujiza ili kuwa viongozi wa nchi na yupo anayetegemea kudra za mwenyezi Mungu ili awe kiongozi bora wa nchi. Ukweli ni kwamba hakuna njia ya mkato ya kupata kitu, si umasikini wala utajiri.
Nayasema haya nikijua kuwa wapo watu wanaotumia muda wao vibaya, wanatumia akili zao na maarifa kwa ajili ya kujikweza, kwa kuwa hawaoni, wanajua kuwa urais ni sawa na embe dodo lililoanguka mtini likaokotwa na mpita njia, basi waendelee kupita wataokota.
Kwamba urais hauna thamani kumbe mtu yeyote akilala usingizi na kuamka asubuhi anaweza kuita mashabiki, wapambe wake na vipaza sauti akatangaza anafaa kuwa rais na ikawa hivyo, basi na iwe.
Kama upo urahisi kiasi hicho cha kuupata nadhani Watanzania wengi wanatumia muda wao vibaya, kwani zipo sifa na taratibu zilizowekwa mahususi na kila chama cha siasa ili kutoa nafasi moja ya mgombea urais.
Kama kila chama kina utaratibu wa kutoa jina moja la mgombea urais, huko wanajua, wanajipima na wanafuata taratibu zao za kupata jina, huo ndio ukweli.
Ni vigumu kuwazuia au kuzuia uhuru wa mtu, kutaka, kutamka na kusema kile anachokitaka, sasa hapo shida inakujaje? Kama kasema anataka kuwa rais kwa nini nyie msioutaka urais mkose usingizi, mkose kufikiria mambo ya msingi? Kama anautaka mwacheni autake.
Mfumo wa vyama vingi vya siasa ndiyo dira ya kuelekea kumpata rais bora na katika harakati hizo ni wazi kuwa ndani ya mchakato huo jina moja lazima liibuke na ushindi, sasa wale wanaoulilia urais kwanini mnawazuia wasiulilie, waacheni waulilie.
Kuulilia urais, kuutamka, kuutangaza, kujizungusha na kuhangaika nao wakati wote hiyo sio shida, shida kubwa ni kuupata. Je, wananchi wako wapi, kwani hawajui aina ya kiongozi wanayemhitaji, hivi rais anayelia na anayejitembeza atajichagua mwenyewe?
Kwa kuwa tunapoteza muda mwingi kuhangaika na vichwa dhaifu vya wanasiasa wanaojisikia na kujiamini kuwa ni bora zaidi ya wapiga kura, basi waendelee kupigana vikumbo, muda ukifika watanyamaza,wataacha kwa kuwa rais wa kweli wa Watanzania yupo.
Rais bora wa Tanzania  yupo, atapatikana kwa amani na kamwe wananchi hawatarajii kumpata kwa nguvu za upanga

No comments:

Post a Comment