Dunia ina mambo ya ajabu ambayo mara nyingine siyo rahisi kuyaamini pale unaposimuliwa kwani unaweza kudhani kuwa ni uzushi au hekaya zisizo na mashiko.
Mshangao mkubwa huja wakati inapothibitika kwamba taarifa hizo ni za kweli kwa kuona au kukutana ana kwa ana na muhusika wa jambo linalozungumzwa. Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa mwandishi wa makala haya, kwani hakuwahi kuamini kwamba katika dunia hii inawezekana mtu akazaa watoto zaidi ya 100. Lakini kukutana ana kwa ana na Mzee Haji Msomi (82), kumethibitisha kwamba inawezekana.
Mzee Msomi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyankumbu, Geita siyo tu kwamba ana idadi kubwa ya watoto, bali hakumbuki vizuri idadi yao na hata ile ya wanawake aliozaa nao.
Hata hivyo inakadiriwa kuwa idadi ya watoto wake ni zaidi ya 100 ambao amewazaa na wanawake zaidi ya 30 mahali na nyakati tofauti. Hivi sasa anaishi na mkewe mdogo, Mariam Joseph (30) ambaye amezaa naye watoto wanne, wa mwisho akiwa na umri wa miaka minne.
Hii inamaanisha kwamba mtoto huyo wa mwisho, Irene Msomi alizaliwa 2010 wakati baba yake huyo akiwa na umri wa miaka 78. Mzee Msomi anasema huyo ndiye kitinda mimba wake na kwamba hana mpango wa kuzaa watoto wengine.
Hata hivyo hakumbuki umri wa mtoto wake wa kwanza. “Mimi sijasoma kwahiyo hata sikumbuki hata huyo mtoto wangu wa kwanza nilimzaa mwaka gani,” anasema mzee huyo.
Mzee Msomi ambaye ni mfugaji maarufu, akiaminika kuwa mmoja wa wamiliki wa makundi makubwa ya ng’ombe, kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa akijishughulisha na uchinjaji na usambazaji wa nyama mjini Geita na sehemu jirani.
Kazi yake hiyo pamoja na sifa ya kuwa na watoto wengi ambao wamesambaa kila kona ya Mji wa Geita na wengine nje ya mkoa huo, ni mambo yanayomfanya kufahamika sana katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria.
Anasema:“Niliamua kuishi maisha hayo kwani afya yangu iliniruhusu na hata wake zangu walinikubali, kwani niliweza kuwahudumia vizuri na hakuna ambaye alilalamika katika hilo”.
Anasema anajivunia kuwa na watoto wengi, kwani kwasasa wengi wao wanafika kumwona, kumjula hali na wanamsaidia licha ya kuwa hakuwalea wala kuwasaidia katika makuzi yao.
Nyumbani kwake
Makazi yake yapo katika Mtaa wa Mbugani, katika kijiji hicho cha Nyankumbu. Ni nje kidogo ya Mji wa Geita mwendo wa dakika ishirini hivi kwa usafiri wa pikipiki.
Ninapofika katika makazi yake nakutana na mzee huyo akiwa ameketi nje ya nyumba yake, huku akiwa amezungukwa na watoto wake watano ambao kiumri wanaonekana kuwa wadogo. Pembeni ameketi mke wake wa sasa, Mariam.
Mara Mzee Msomi ananikaribisha: “Karibu tupo, karibu kiti uketi, karibu sana”. Baada ya kusalimiana naya pamoja na waliomzunguka ninaketi kwenye kiti nay eye anaendelea…….ehe! unasemaje mama, umetokea wapi na una shida gani tukusaidie?”
Mazungumzo yake yanaonyesha kuwa ni mtu mwenye shauku ya kufahamu kile kilichonifikisha katika makazi yake. Maswali yake yananipa fursa ya kujitambulisha mimi ni nani na ninakotokea na baada ya hapo naanza kumuhoji kwa kutaka kufahamu historia yake na kubwa zaidi idadi ya watoto na ile ya wake zake.
Mzee Msomi anapokea maswali yangu kwa mguno na kicheko kidogo. “….kwakweli nina watoto wengi hata idadi sikumbuki, maana najua nimezaa watoto wengi sana kiasi ambacho inanipa shida ya kujua idadi yao”alisema Msomi huku akitabasamu.
Msomi anasema kwa kukisia tu, watoto ambao anawakumbuka ni 40 japokuwa anakiri kwamba wanazidi idadi hiyo. “Nakumbuka watoto 40 ila wengine siwakumbuki kwasababu nilizaa na wake wengi, na wengine walitaka tu kuzaa na mimi kisha wakaondoka na watoto wao,” anasema.
Kisa cha watoto wengi
Anaeleza kuwa wakati akiwa kijana alibahatika kuozeshwa mke na baba yake mzazi na kwamba katika muda wa ndoa yao ya miaka 8, walizaa watoto saba. “Baada ya kuachana naye nikaoa mke wa pili ambaye nilifunga naye ndoa na nikazaa naye watoto wanane,” alisema Msomi.
Anasimulia kwamba baada ya kuachana na mke wake wa pili, alianza kuoa kila mwaka kwa maana ya kwamba kila baada ya mwaka mmoja alioa mke mpya na akishazaa naye tu, alikuwa anaoa mwingine.
Anasema kitendo cha kuoaoa kiliwakwaza baadhi ya wake zake, hivyo waliamua kumuacha na kuondoka na watoto wao. “Waliokuwa wakichoka waliamua kuniacha wenyewe, tena kwa amani bila ugomvi”alisema Msomi.
Anasema aliendelea kuishi maisha hayo ya kuoa na kuacha na kwamba kwa mwenendo huo hawezi kukumbuka idadi kamili ya wake aliozaa nao, wala majina yao.
“Mimi sijasoma hivyo hata sikumbuki nilioa wake wangapi eti Mariam unaweza kunikumbusha,”alisema huku akimuuliza mkewe mdogo ambaye naye hakuweza kufahamu idadi ya wake wenzie.
Msomi anasema idadi ya inaweza kuwa zaidi ya 30 na kwamba aliamua kufanya hivyo (kuoa na kuacha) kwani afya yake ilikuwa inaruhusu na na dini yake pia. “Ni haki yangu kwasababu kila mtu ana haki ya kuishi anavyotaka, isipokuwa tu asivunje sheria.
Watoto wako wapi?
Msomi anaeleza kuwa watoto wake wako maeneo tofauti ambayo ni Geita mjini na wengine vijijini, jijini Dara es Salaam na mikoa mingine nchini.
Hapa nyumbani ninakaa na watoto 30, wengi ni wakubwa wanajitegemea na ninaokaa nao ni watoto niliozaa na wake zangu wanne ambao wao waliamua kuniletea niwalee mwenyewe.
Anasema watoto wake wote hawasomi ila wanafanya shughuli zao ndogondogo, huku akijivuna kwamba kwa kazi zao wanamsaidia kwani wanamletea zawadi nyingi.
Mzee Msomi anawapa sifa wake zake wote aliozaa nao kwa kuamua kumsaidia kulea na kusomesha watoto.
“Kwakweli nawashukuru wake zangu kwani hawana kinyongo na mimi na wanapendana sana, kuna mke wangu yuko Dar es Salaam ambaye nilizaa naye watoto 10, yeye aliamua kuishi na watoto wangu na anawasomesha tena shule za gharama,” alijighamba.
Kauli za mtoto, mke
Mmoja wa watoto wake, Hassan Msomi (21) anamtupia lawama baba yake kwa kitendo cha kuzaa watoto na kwamba hali hiyo imesababisha wengi wao kukosa fursa ya kupata elimu na malezi bora.
“Mimi sifurahii tabia ya baba yetu, wengine hapa hata mama zetu hatuwajui anatuambia tu mama yako yuko Mwanza, mara wengine yuko Musoma, kweli mimi sijasoma nahangaika tu mjini hapa,”anasimulia Hassan.
Anasema hawafahamu baadhi ya ndugu zake na kwamba anasikia tu kuwa wengine wapo Geita na kwamba baadhi ya dada zake wanafanya biashara ya ngono kutokana na ugumu wa maisha.
Kuhusu idadi ya ngugu, Hassan anasema kwa hesabu za haraka, anaowafahamu wanafikia 100 na kwamba kuna kila dalili kwamba wanazidi idadi hiyo.
“Hata ndugu zangu wakubwa huwa wanasema kwamba baba ana watoto zaidi ya 100 na huwa wanakuja hapa nyumbani kumsalimia na wanamletea zawadi tena mara kwa mara,” anasimulia Hassan.
Kwa upande wake, Mariam yeye anasema anajisikia vema kuolewa na mzee huyo na anafurahia kuishi naye. “Najua mimi bado mdogo siendani na umri wa mume wangu, ila mimi nimempenda licha ya kuwa ana wake wengi na watoto wengi,” anasema Mariam.
Anasema mume wake alimwambia ana watoto wengi ila hakumbuki idadi yao na kwamba mara nyingi huwa wanafika na kujitambulisha kwamba ni watoto wake.
Mariam anasema watato waliowahi kufika nyumbani hapo ni zaidi ya 40, mbali na 30 anaoishi nao. “Juzi alikuja mtoto wake wa kike ambaye alikuwa anamtafuta baba yake, tulikaa naye hapa kwa wiki 3 na baadaye aliondoka,” anasema Mariam.
Wataalam wa uzazi
Wataalamu wa masuala ya uzazi wanasema mwanamume anaweza kuzaa watoto 15 kwa mke mmoja, lakini wakaongeza kuwa aikiwa ni kwa wanawake tofauti naweza kuzaa maelfu ya watoto.
Dk. Nelson Bukuru ambaye ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale alisema wakati ukomo wa uzazi kwa mwanamke ni miaka 45, kwa mwanaume ni miaka 75 lakini zaidi ya umri huo mbegu ambazo huzalishwa na mwanaume huwa ni hafifu.
Dk. Bukuru ambaye ni mtaalamu wa uzazi, anasema kwa maana hiyo Mzee Msomi alikuwa na uwezo wa kuzaa watoto wengi kutokana na kuzaa na wanawake tofauti ambao kama
VIA-MWANANCHI
No comments:
Post a Comment