Pages

Sunday, 20 July 2014

RAIS KIKWETEA KUFUNGUA MKUTANO WA 45 WA UMOJA WA MABUNGE JUMUIYA YA MADOLA CPA

Anne Makinda, Rais wa CPA Kanda ya Afrika
RAIS Jakaya Kikwete, anatazamiwa kufungua mkutano wa 45 wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) Kanda ya Afrika unaojumuisha wajumbe 500 kutoka nchi 17 wanachama.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na mkutano huo ni chaguzi za ukanda huo kama zinakuwa huru na haki pamoja na sababu za kutokea ugomvi mara zinapomalizika.
Mkutano huo utaangalia sababu za uchumi wa nchi hizo kuonekana kukua kwa kasi huku hali za wananchi wake zikiendelea kuwa duni kiasi cha baadhi ya wananchi kwenye nchi kufa kwa kukosa chakula.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani hapa, Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, ambaye pia ni Rais wa CPA Kanda ya Afrika alisema mkutano huo utafunguliwa rasmi Julai 24, ingawa vikao mbalimbali vya kiutendaji vimeanza kuanzia jana.
Alisema kuwa chombo hicho hufanya mkutano wake mara moja kwa mwaka ambapo nchi inayojitolea kuandaa wa mwaka unaofuata hupewa fursa ya kukiongoza kwa mwaka mmoja. Baada ya Tanzania, Spika wa Bunge la Lesotho, Sephiro Motanyane, atakabidhiwa rasmi uongozi wa chombo hicho.
Alisema kuwa wanatarajia kujadili changamoto zinazozikabili nchi hizo ambapo katika hatua ya awali watakaa kulingana na kanda wanazotoka kwa kile alichoeleza kuwa kila eneo lina changamoto zake ambapo baadaye watawasilisha kwenye mkutano wa pamoja.
“Nchi zetu (wanachama wa CPA) zinakua kiuchumi, lakini zote bila kubagua wananchi wake bado wana hali duni, wanakabiliwa na njaa, utapia mlo, vita. Dalili ya kukua, uchumi unaonekana unapaa kitakwimu, lakini mbona watu wetu wana njaa? Tunataka kushirikiana kumaliza haya.
“Tunataka kujadili kuona chaguzi zetu ni huru kama tunavyotaka, maana ukimalizika uchaguzi, magomvi yanaanza, je ni kanuni zetu hazifuatwi au tatizo ni nini?” alisema Spika Makinda.
Alisema kuwa pia wataangalia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambapo mjadala huo utawahusisha watoa mada kutoka Bunge lao la vijana ambalo lina muhula wa tatu sasa toka lianzishwe.
Spika Makinda, alisema kuwa kwa miaka 10 sasa Tanzania inaongoza sekretarieti ya CPA baada ya Zimbabwe kujiondoa kwenye umoja huo ambapo wanatazamia kujenga makao makuu na kitega uchumi eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment