Pages

Saturday, 26 July 2014

MLEBANONI MBARONI KWA KUHUJUMU UCHUMI

RAIA wa Lebanon, Mohamed Attwi akijifunika  asionekane
RAIA wa Lebanon, Mohamed Attwi (27), amepandiswa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, akikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kuisababishia hasara ya zaidi ya sh bilioni 2 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akiwasomea mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Tumaini Kweka, alidai kuwa Attwi alitenda makosa hayo kati ya Novemba 3, 2013 na Julai 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kweka alidai kuwa katika tarehe isiyofahamika mwaka 2013, mtuhumiwa huyo aliingiza nchini vifaa vya kielektroniki na mawasiliano vyenye No. 2143281001701 bila kibali kutoka TCRA.
Aliendelea kudai kuwa katika tarehe tofauti mtuhumiwa alifanikiwa kuvisimika vifaa hivyo ambavyo havijathibitishwa na TCRA na kuendelea kuendesha mawasiliano bila kibali.
Aliileza mahakama kuwa kwa sasa wanasubiri kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ili kesi hiyo ikasikilizwe Mahakama Kuu kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za kuhujumu uchumi zenye kiwango kinachozidi sh milioni 10.
Wakili wa mshitakiwa, Jamhuri Johnson, aliomba mahakama impe dhamana mteja wake kwa kuwa ana haki kwa mujibu wa sheria.
Upande wa jamhuri ulikiri shitaka hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria, lakini kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, haina uwezo wa kutoa dhamana.
Mshitakiwa amepelekwa rumande hadi Agosti 11, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa

No comments:

Post a Comment