Pages

Saturday, 19 July 2014

DK.SHEIN ARIDHISHWA NA USHIRIKIANO NA ISRAEL

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Israel, Gil Haskel aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar jana kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar na Israel zina kila sababu za kuimarisha ushirikiano wao ambao wakati wote umeonesha mafanikio kwa kila upande. 
Akizungumza na Balozi wa Israeli nchini Tanzania anayemaliza muda wake, Gill Haskel, Dk. Shein, alisema ushirikiano kati ya Zanzibar na Israeli umeshuhudia matokeo mazuri hususan katika sekta za afya na kilimo.
 
Alieleza kuwa chini ya ushirikiano huo Israeli imekuwa ikisaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya afya kupitia Mpango wa Huduma ya Afya kwa Watoto ambapo hadi sasa watoto zaidi 200 hasa wenye matatizo ya moyo wamefaidika na mpango huo.  

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ingependa kuona ushiriki zaidi wa Israeli katika kuunga mkono mpango wa serikali kuimarisha kilimo hasa katika kuwajengea uwezo watafiti wa Zanzibar na kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo nchini.
 
Alifafanua kuwa chini ya mpango huo wa serikali, moja ya lengo ni kujitosheleza kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji kupitia uimarishaji wa kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo. Aliongeza tangu kuanza kwa mpango huo uzalishaji katika kilimo cha mpunga umeongezeka mara tano hivyo lengo la kufikia angalau asilimia 50 ya mahitaji ya chakula ifikapo mwaka 2015/2016 linaelekea kufikiwa.
 
Sambamba na kilimo cha mpunga Rais alimueleza Balozi huyo kuwa fursa pia zimeelekezwa katika kuwasiaidia wakulima katika mazao mengine ikiwamo kilimo cha mbogamboga zikiwamo tungule asili ambazo zinalimwa maeneo kame.
 
Dk Shein aliiomba Serikali ya Israel kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maafa yakiwemo katika usafiri wa majini.
 
Balozi Haskel ambaye alikuwa amefuatana na mke wake alimhakikishia Dk Shein kuhusu azma ya serikali ya nchi yake ya kuendeleza ushirikiano na misaada yake kwa Zanzibar.
 
Alieleza kuwa anaondoka huku akiwa anaamini kuwa katika kipindi chote alipokuwa akiitumikia nchi yake nchini ameweza kuimarisha uhusiano kati ya Israel na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment