UTARATIBU mpya wa kudhibiti changamoto ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam uko mbioni kutangazwa.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Ofisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Asteria Mlambo, alipozungumza na waandishi wa habari.
Mradi wa DART unalenga kuimarisha huduma za usafiri na kuwa za kisasa zaidi pamoja na kupunguza msongamano ambao umekuwepo kwa kipindi kirefu.
Katika awamu ya kwanza, mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara maalumu ya umbali wa kilometa 20.9 kutoka
Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kuanzia Faya hadi eneo la Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi njia panda ya Morocco.
Akizungumzia mahitaji ya utaratibu huo mpya, alisema gari zote zitakazotumia njia hizo mpya hazitatakiwa kuzidi mwendo wa kilometa 50 kwa saa hasa katika barabara ya Morogoro ambapo mradi huo unakaribia kukamilika.
Akielezea zaidi alisema magari hasa daladala hazitaruhusiwa kusimama njiani na pia itakuwa marufuku kufanya biashara ndogo ndogo au biashara ya aina yoyote katika maeneo ya njia hizo.
“Kwa sasa tunaangalia maeneo ya muda ambayo daladala zitaruhusiwa kusimama,” alisema na kuongeza kuwa taratibu zote zimekamilika na kuwa polisi wataanza kuhakikisha kuwa utaratibu huo unafuatwa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa ofisa huyo wa DART, kupaki magari au kufanya biashara katika maeneo ya waenda kwa miguu haitaruhusiwa na watakaokiuka watakumbana na adhabu kali.
“Napenda pia kuwataarifu wafanyabiashara kuacha kupaki magari ya mizigo katika njia kuu na kupakua au kupakia mizigo,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa itakuwa marufuku pia kupaki magari katika njia za pembeni na wala pikipiki hazitaruhusiwa kupita katika njia za waenda kwa miguu.
Alisema utaratibu huo utasimamiwa na kufuatiliwa na vyombo mbalimbali kama DART, askari wa usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) pamoja na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads)
No comments:
Post a Comment