Thursday, 26 June 2014

SISTA ALIYEUAWA NA MAJAMBAZI KUAGWA LEO

 Sista wa Kanisa Katoliki, Clencensia Kapuli aliyeuawa na majambazi na kuporwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho bado hakijafahamika, anatarajiwa kuagwa leo katika Parokia ya Mtakatifu Gaudence Makoka, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwenyeheri Anuwarite, Carlos Mgumba alisema ibada ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa sita mchana shuleni hapo, kabla ya mwili kusafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko.
“Nashindwa kujizuia kila nikifikiria jinsi walivyomuua kikatili, sista, alikuwa mpole na mnyenyekevu…Wametumia nguvu kubwa kama shida yao ilikuwa ni fedha wangeweza hata kuchukua bila kutumia silaha, wametuachia pigo kubwa kwa shule yetu, wamemwonea tu,” alisema huku akitokwa na machozi. Mgumba alisema katika miaka miwili na nusu aliyofanya naye kazi, Sista Kapuli alisaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya shule kutokana na utendaji kazi wake uliotawaliwa na uaminifu.
“Nakumbuka siku hiyo tulikuwa pamoja asubuhi kwa mipango ya malipo ya mishahara ambayo kwa kawaida tunalipa moja kwa moja kwenye akaunti za walimu, saa sita hivi mchana aliniaga anakwenda benki kuchukua fedha za (petty cash) matumizi madogo ya shule,” alisema.
Alisema akiwa anaendelea na kazi zake, ndipo alipopigiwa simu na kujulishwa kuhusu tukio hilo la mauaji lililotokea eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam hukuna dereva Mark Mwarabu kukatwa kidole gumba kwa risasi.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa sekondari hiyo, James Sweya alisema marehemu alikuwa karibu naye kwa sababu, yeye anasomea mchepuo wa biashara hivyo alikuwa akimsaidia kumpa mwongozo wa mambo ya uhasibu.
Mwanafunzi mwingine, Evelyn Kiwenge alisema Sista Kapuli alikuwa mwenye upendo wa aina yake msaada kwa maisha ya wanafunzi wengi katika sekondari hiyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema juzi kuwa tayari kimeundwa kikosi kazi ili kufuatilia tukio hilo na akiahidi kwamba atahakikisha wote waliohusika wanasakwa na kutiwa mbaroni.
Alisema majambazi hayo yaliua na kupora Sh20 milioni lakini hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa majambazi hayo yalipora Sh10 milioni.
Sista Kapuli aliuawa akiwa ameongozana na wenzake, Sista Brigita Mbaga na dereva Mwarabu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux walikuwa wakitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City kuchukua fedha.
Baada ya kufika Ubungo kwa lengo la kulipa deni la chakula katika duka la Thomas Francis, ndipo walitokea majambazi wawili wakiwa na pikipiki ambayo haikusomeka namba mmoja wao akiwa na bunduki aina ya SMG na kumpiga risasi ya kidole gumba cha mkono wa kulia Mwarabu kisha kumgeukia Sista Kapuli na kumuua kisha kuondoka na fedha zilizokuwa kwenye pochi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!