Friday, 13 June 2014

NI BAJETI YA LALA SALAMA!


BAJETI Kuu ya Serikali ya Sh trilioni 19.87, imewasilishwa jana bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, huku ikiwabana wananchi katika bidhaa na huduma za starehe, na kipaumbele kikubwa kikiwa elimu.


Aidha, katika Bajeti hiyo, badala ya Serikali kupata fedha kutoza kodi bidhaa za muhimu kwa wananchi kama mafuta, safari hii, wananchi hawajaguswa katika huduma na bidhaa muhimu kwao, na badala yake fedha nyingi zinatarajiwa kukusanywa baada ya kufuta misamaha ya kodi.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri Saada, aliweka wazi kuwa ni Bajeti ya ‘lala salama’, pale aliposema kuwa ndiyo Bajeti ya mwisho, katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II).
“Mheshimiwa Spika, Awamu ya Pili ya Mkukuta inafikia tamati Juni 2015, hivyo Bajeti hii ni ya mwisho katika utekelezaji wa Mkukuta II. Aidha, Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yametumika kama sehemu ya mikakati yetu ya kupunguza umasikini yanafikia tamati mwaka 2015,” alisema Waziri Mkuya.
Ingawa Waziri Mkuya hakuweka wazi, lakini Bajeti hiyo pia ndiyo ya mwisho itakayotekelezwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Bajeti ijayo ya 2015/16, Serikali iliyopo madarakani itapata fursa ndogo ya kutekeleza sehemu tu ya bajeti hiyo, na sehemu itakayobakia, itatekelezwa baada ya kupatikana kwa Rais wa Awamu ya Tano, baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mipango mingine inayopaswa kumalizika kabisa au kwa sehemu kubwa wakati wa utekelezaji wa Bajeti hiyo, ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010-2015 na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 utafikia tamati Juni 2016.
“Kazi iliyo mbele yetu ni kutafuta jinsi masuala ya kupunguza umasikini, yatakavyooanishwa katika mikakati na mipango yetu baada ya Juni 2015, wakati tunaelekea kuhitimisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano mwaka 2016,” alisema Mkuya. Maumivu
Alisema Serikali itaongeza ushuru wa vinywaji baridi kutoka Sh 91 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 9 kwa kila lita. Pia itaongeza ushuru wa bidhaa kwenye juisi iliyotengenezwa kwa matunda yaliyozalishwa hapa nchini kutoka Sh 9 kwa lita hadi Sh 10 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh moja tu kwa lita. Pia itaongeza ushuru wa bidhaa kwenye juisi iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka Sh 110 kwa lita hadi Sh 121 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 11 kwa lita.
“Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani, hautaongezeka,” alisema Mkuya.
Kwa upande wa bia, ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa mfano kibuku, utaongezeka kutoka Sh 341 kwa lita hadi Sh 375 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 34 kwa lita.
Ushuru wa bia nyingine zote, utaongezeka kutoka Sh 578 kwa lita hadi Sh 635 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 57 kwa lita.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi, kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utaongezeka kutoka Sh 160 kwa lita hadi Sh 176 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 16.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi, kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka Sh 1,775 kwa lita hadi Sh 1,953 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 178 kwa lita.
Ushuru wa vinywaji vikali, utaongezeka kutoka Sh 2,631 kwa lita hadi Sh 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 263 kwa lita.
“Marekebisho ya viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: Sigara zisizokuwa na kichungi, zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini, kwa kiwango cha angalau asilimia 75, utaongezeka kutoka Sh 9,031 hadi Sh 11,289 kwa sigara 1,000.
Hiyo ni sawa na ongezeko la Sh 2.25 kwa sigara moja,” alisema.
Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, ushuru wake utaongezeka kutoka Sh 21,351 hadi Sh 26,689 kwa sigara 1,000 ikiwa ni ongezeko la Sh 5.30 kwa sigara moja.
Ushuru kwa sigara nyingine, zenye sifa tofauti na zilizotajwa hapo juu, kwa mujibu wa Waziri Saada, utaongezeka kutoka Sh 38,628 hadi Sh 48,285 kwa sigara 1,000, sawa na Sh 9.65 kwa sigara moja. “Ushuru wa sigara aina ya ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30,” alisema.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!