Sunday, 22 June 2014

MAMA KIKWETE AWATAKA WAZAZI NA WALEZI KUWEKEZA KATIKA ELIMU YA WATOTO WAO

 index


Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wazazi na walezi wilayaniLindi mjini  wametakiwa kuwekeza katika elimu ya  watoto wao kwa kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati kwani  elimu ni ukombozi wa maisha na kuolewa katika umri mdogo kwa watoto hao hakutawasaidia kimaisha.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea  kwa nyakati tofauti  na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi yaliyopo kweye kata za Chikonji, Tandangongoro na Ng’apa  wilaya ya Lindi mjini.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema  ni jukumu la mzazi na mlezi kusimamia elimu ya mtoto wake pamoja na kumpa malezi mazuri kwa  kufuata malezi ya zamani yanayoendana na mila na utamaduni wa mtanzania  kwani hivi sasa kutokana na utandawazi mienendo ya vijana wengi siyo mizuri.
MNEC huyo pia aliwataka watoto waliofika kumsalimia mara baada ya kumaliza mkutano wake wa ndani na viongozi hao wa CCM kusoma kwa bidii na kuacha tabia ya utoro kwani elimu pekee  ndiyo itakayowakwamua na hali ngumu ya maisha.
Aidha Mama Kikwete  aliwahamasisha viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kujiunga katika vikundi mbalimbali vya maendeleo  na kuandika maandiko ya kibiashara ili wapate mkopo kutoka Serikalini  na kuweza kufanya miradi kama ufugaji wa kuku, mamalishe, ufundi seremala, kwa kujishughulisha  na biashara hizo  watakuwa wamejikwamua kiuchumi.
“Mkijiunga katika vikundi vya ujasiriamali mtaweza kukopa fedha kutoka Serikalini jambo la muhimu mkumbuke kuwa fedha hizi  hampewi bure  mnatakiwa kuzirudisha ili na wenzenu waweze kukopa”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa Afya aliwahimiza  kina mama kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ikiwemo  saratani ya matiti na shingo ya kizazi ambayo inatibika ikiwa  itagundulika mapema mgonjwa atapata matibabu na kupona.
“Hivi sasa kuna maradhi  mengi ikiwemo saratani ya matiti na shingo ya kizazi msiogope kwenda kupima na kujua  afya zenu. Nanyi kinababa wahimize wake zenu  wakapime ugonjwa huu, mkiona dalili  wawapeleke Hospitali mapema  kwani ugonjwa huu unatibika kama mgonjwa atawahi   mapema kupata matibabu”, alisisitiza.
Alimalizia kwa kuwataka viongozi hao kuonyesha mfano kwa wananchi kwa kujenga nyumba bora za matofali ya kuchoma na kuezeka kwa bati na siyo za miti kwani moja ya sera ya CCM  ni kuwahamasisha wananchi kutunza  mazingira na kutokukata miti hovyo.
Akiwa katika Kata ya Chikonji MNEC huyo alikagua mradi wa maji wa Kwamtokama na kujionea maendeleo ya  mradi huo ambao ukikamilika utawanufaisha wananchi wapatao  elfu saba kutoka  vijiji vya Jangwani, Nanyanje , Chikonji Kusini na Kaskazini.
Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya matawi ya CCM  katika matawi ya Chikonji Kusini na Kaskazini,Nandambi, Kilolombwani na Cheleweni kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya ndani na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!