Monday 23 June 2014

KIWANDA CHA KICHINA CHABAINIKA!

 Raia mmoja wa China anadaiwa kumiliki kiwanda bubu cha samani na vifaa vingine vya ujenzi katika eneo la Tabata-Segerea, Mtaa wa Migombani, Dar es Salaam.
Kiwanda hicho kinachoitwa L&J Engineering kilichopo katikati ya makazi ya watu, kinaendesha shughuli zake kwa usiri, bila kutoa stakabadhi na hata baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanadhani nyumba inayohusika ni makazi tu ya Wachina.

Mwandishi wetu alinunua mito miwili iliyotengenezwa kwa pamba, kila mmoja ukiuzwa kwa Sh7,000 lakini alipodai risiti aliambiwa kwamba hawatoi risiti kwa bidhaa ndogondogo.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kiwanda hicho kimeliingizia hasara ya Sh30.4 milioni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutokana na wizi wa umeme.
Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Ahmed Mmingwa alisema baada ya kufanya tathmini katika mita ya nyumba kilipo kiwanda hicho, walibaini kuwa imechezewa.
“Tumepata hasara ya Sh30,388,853.42 kutoka katika kiwanda hicho pekee. Sasa tutawapelekea barua ili walipe deni hilo,” alisema.
Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Ilala, John Chirare aliyegundua kuchezewa huko, alisema baada ya kufuatilia usajili, walibaini kuwa mita hiyo imesajiliwa kwa jina la Dk Kwayo kama nyumba ya kuishi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Masoko wa L&J Engineering, Meshack Lakati alisema walipanga katika nyumba hiyo siku nyingi na mita haikuwahi kubadilishwa.
Alisema inawezekana mita ndiyo yenye tatizo na kwamba wao hawajafanya hila zozote za kutumia umeme huo kwa shughuli zao. Alisema bidhaa zinazotengenezwa kiwandani hapo hazitumii umeme mkubwa kwa sababu ni za kawaida ambazo hutengenezwa pia katika maeneo mengine.
“Kampuni yetu inalipa ankara ya umeme kila mwezi, hatujawahi kuchezea mita. Lakini kwa kuwa Tanesco wamebaini kuwa mita haiko sawa, basi itakuwa na tatizo kwa vile imetumika muda mrefu bila kubadilishwa,” alisema.
Licha ya tatizo hilo la mita, kiwanda hicho kinadaiwa kuendeshwa kinyemela bila ya kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela). Mwandishi wetu alipitia usajili wa kampuni hiyo Brela ili kujua imesajiliwa kwa shughuli zipi, lakini haikuonekana.
Hata hivyo, Lakati alipinga madai ya kutokusajiliwa akisema kiwanda hicho hakiwezi kufanya biashara zao bila ya kuwa na usajili kutoka Brela. Hata hivyo, alipotakiwa kutaja namba ya usajili alisema hahusiki na hilo kwa kuwa lipo katika mamlaka nyingine
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!