Friday 20 June 2014

CHANZO CHA KUUGUA MKANDA WA JESHI



Katika mwendelezo wa safu hii kuhusu madhara ya ngozi, leo nitajibu swali la Thomas Lyatuu kuhusu ugonjwa unaojulikana kama mkanda wa jeshi au kwa kitaalamu herpes zoster.

Maradhi haya kwa jina jingine huitwa shingoz husambazwa na virusi vinavyoitwa varicella zoster.
Maradhi haya hujitokeza ghafla yakiambatana na homa kali pamoja na malengelenge ambayo hutokea kama mstari kwenye eneo husika la ngozi.
Mara nyingi maradhi haya huonekana kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga kama vile wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) ama wale wanaotibiwa maradhi ya saratani na wenye lishe duni.
Virusi vya varicella zoster huwa vinasafiri kutoka kwenye ngozi na kufuata mwelekeo wa mishipa ya fahamu. Vinapofika kwenye maeneo maalumu ya mishipa ya fahamu kwa jina la sensori ganglia huwa vinaweka makazi yao ya kudumu hapo.
Hukaa mahali hapo kwa muda wote wa maisha ya binadamu huyo. Inapotokea binadamu huyo akapata tatizo la kiafya linalosababisha kinga ya mwili kushuka, virusi hao huanza kushambulia. Mbali na VVU, mambo mengine yanayoweza kusababisha kinga kupungua ni msongo wa mawazo, maumivu ya mwili, majeraha mwilini au maradhi ya saratani.
Kinga hiyo inapopungua, virusi hao huanza kushambulia mwili kwa kuonyesha madhara kwenye ngozi na hapa ndipo unapopata mkanda wa jeshi.
Mkanda wa jeshi huathiri zaidi watu wazima na ni mara chache sana kutokea kwa watoto. Maradhi huanza na dalili za maumivu makali sana.
Wataalamu wa mambo ya maumivu wanayaelezea kuwa ni makubwa sana pengine yanashika nafasi ya pili baada ya maumivu yatokanayo na uzazi.
Yakiambatana na maumivu haya, maradhi haya pia hujitokeza na hali ya kupotea kwa fahamu kwenye eneo lililoathirika pamoja na malengelenge yaliyojikusanya.
Haya hujitokeza siku chache yakitengeneza mfano wa mstari wenye mkusanyiko wa malengelenge kwa kufuata njia ya mishipa ya mfumo wa fahamu.
Namna moja ya kutofautisha maradhi haya na mengine ya ngozi ni kuwa karibu mara zote (asilimia 99.9) huwa hayakatizi sehemu ya katikati ya mwili
Maradhi haya hutokea upande mmoja wa mwili huku yakifuata mwelekeo wa mfumo wa fahamu.
Mara nyingi maradhi haya huambatana na homa kali pamoja na maumivu ya misuli ya mwili. Maradhi haya hushambulia zaidi maeneo ya kifua.
Wagonjwa wengi wanaopata maradhi haya huweza kupata nafuu kwa kutibu tu dalili za ugonjwa.
Wagonjwa wenye umri mkubwa mara nyingi huendelea kusikia maumivu hata baada ya kutibiwa.
Maradhi haya hutambulika kwa mwonekano wake. Tabibu au mtaalamu wa afya husikiliza historia ya maradhi haya na pia hutazama jinsi yanavyoonekana kwenye ngozi.
Sehemu zenye vifaa vya upimaji huenda hatua za ziada na kuotesha vimelea vya maradhi.
Maradhi haya hutibiwa kwa kuhakikisha mgonjwa anapata mapumziko ya kutosha na kupewa dawa za kutuliza maumivu.
Mgonjwa hupewa dawa maalumu za kuua virusi muda mfupi baada ya dalili za ugonjwa kuonekana kati ya saa 24 hadi 72.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!