Watu watatu wamefariki dunia wakiwamo wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, ambao walipoteza maisha baada ya kuzama kwenye bwawa la samaki.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema jana kwamba wanafunzi Michael Tarimo (20) na Albert Shenkalwa (23) walifariki dunia juzi baada mtumbwi waliokuwa wakiutumia kupinduka kwenye bwawa maalumu la samaki linalosimamiwa na Hospitali Teule ya Ifisi eneo la Mbalizi jijini hapa.
Msangi alisema bwawa hilo ni sehemu ya ‘Zoo ya wanyama’ inayosimamiwa na hospitali hiyo ambapo watu mbalimbali wanafanya utalii kutembelea na kujionea wanyama wa aina mbalimbali pamoja na kupanda mtumbwi kwenye bwawa dogo.
Alisema wanafunzi hao walikuwa wakisomea stashahada ya biashara na kwamba walikwenda huko pamoja na wenzao 12, kwenye ‘pikiniki.’ Alisema pamoja na kuangalia wanyama pia walikwenda kwenye bwawa linalotunza samaki ambako walipanda mtumbwi lakini ulijigeuza ghafla na walishindwa kuogelea.
“Kwa kawaida katika bwawa hilo, watu hawaruhusiwa kuogelea isipokuwa kuingia kwa mtumbwi,’’ alisema. Kuhusu kifo cha mtu wa tatu, Kamanda Msangi alisema mkazi wa Kijiji cha Mpolo-Igawa, wilayani Mbarali Anaheri Lazaro (43) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji. Msangi alisema uchunguzi wa polisi uligundua kwamba silaha iliyotumika ni gobori baada ya kuokotwa golori moja eneo la tukio.
Alisema chanzo cha mauaji kinachunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa Kituo cha Afya Igurusi
No comments:
Post a Comment