Sunday, 4 May 2014

VIGOGO WA BARCLAYS WAPANDISHWA KIZIMBANI

HATIMAYE Meneja wa Benki ya Barclays tawi la Magomeni jijini Dar es Salaam, Alune Kasililika (38), na Meneja wa Benki hiyo Neema Batchu (26), ni miongoni mwa watu saba waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kwa wizi wa sh milioni 390.2, mali ya benki hiyo.

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika mahakama hiyo, wakituhumiwa kwa wizi wa fedha hizo kwa kutumia silaha.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi ni Kakame Julius (38), Iddy Khamis (32), Sezary Msolopa (31), Boniphace na Muumba (29) na Ruth Macha (30).
Wakili mwandamizi wa serikali, Tumaini Kweka, akisaidiwa na Mwanaamina Kombakono, mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba, alidai kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili.
Katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa katika tarehe tofauti zisizofahamika, wakiwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la wizi.
Wakili Kweka alisema katika shitaka la pili, watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa  Aprili 15 mwaka huu, wakiwa katika eneo la  benki hiyo tawi la Kinondoni jijini Dar es Salaam, waliiba fedha taslimu sh milioni 390.2, dola za Kimarekani 55,000 na Euro 2,150, mali ya Barclays.
Aliongeza kuwa kabla ya kufanya wizi huo, walimtishia kwa silaha Anifah Ahmad na Anna Tegete ambao ni wafanyakazi walinzi wa benki hiyo.
Hata hivyo, washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na wakili Kweka aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa na kutaka washitakiwa wafungiwe.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Mwaseba alisema kwa mujibu wa sheria, shitaka la pili halina dhamana, hivyo aliamuru washitakiwa wapelekwe rumande hadi kesi yao itakapotajwa tena   Mei 15, mwaka huu
TZ- Daima

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!