SHIRIKA la Kutetea Uhai wa Binadamu (Prolife) limesema chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi iitwayo Gardasil imegubikwa na hofu kutokana na baadhi ya wataalamu kueleza kuwa nguvu ya dawa hiyo hudumu kwa miaka mitano tu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Shirika hilo, Emil Hagamu, alisema mkanganyiko huo unatoa hofu kwa wananchi hasa wasichana wanaopaswa kutumia chanjo hiyo.
Alisema licha ya baadhi ya madaktari na watafiti kueleza kuwa chanjo hiyo itadumu kwa miaka mitano, lakini hakuna anayejua kinga hiyo itadumu zaidi kwa muda gani na wala kuelezwa madhara yake.
Alisema ingawa serikali imepanga kuzindua kampeni katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Kilimanjaro baada ya kufanyiwa majaribio mkoani Mwanza, ni vema juhudi zichukuliwe ili kubaini athari za chanjo hiyo.
Hagamu alisema ni chanjo mpya inayokusudia kuondoa aina nne ya virusi viitwavyo ‘Human Papilloma Virus’ ambavyo vinasadikiwa kuwa chanzo cha saratani ya shingo ya kizazi.
“Hata hivyo chanjo hii siyo salama, kwa kweli kama kuna jambo linalofahamika kuhusu chanjo ya Gardasil ni kuwa imegubigwa na utata mtupu.
“Marekani kuliwahi kuripotiwa na Shirika la Judicial Watch la Washington kuwa chanjo hiyo ilihusishwa na vifo vya wasichana watatu, mdogo kabisa alikuwa na umri wa miaka 12, hivyo serikali iwe makini katika kuipokea,” alisema.
No comments:
Post a Comment