Picha hii haihusiani na habari husika!
BAADA ya gazeti la Tz Daima kuandika makala kuhusu mtoto Hamad Nuruabeid (4) anayeishi Mkata Mashariki, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga ambaye analisha familia yake kwa kuokota chupa tupu za maji, ameanza kupokea misaada mbalimbali.
Baadhi ya watu walioguswa na kutoa vitu mbalimbali ni Michael Mburuma, mkazi wa Kijichi, Dar es Salaam aliyetoa kiroba cha unga cha kilo 25 pamoja na mavazi.
Akizungumza na Tanzania Daima baada ya kukabidhi mchango huo, Mburuma alisema aliguswa na makala hiyo na kuamua kutoa msaada kwa mtoto huyo.
“Ile makala ilinigusa sana, hasa baada ya wewe mwandishi kuandika maisha ya mtoto huyo na kuomba kuungana na sisi katika kuhakikisha anapata msaada, endelea kuwa na moyo huo na usaidie watoto wengine,” alisema.
Wengine waliofika ofisi za gazeti hili kutoa msaada ni Mohamed Haji, mkazi wa Zanzibar aliyetoa sh 70,000 pamoja na viatu, huku Rosemary Madeu akitoa msaada wa sh 50,000.
Wengine ni Alec Rwongezibwa aliyechangia sh 20,000, Said Hussen alichangia sh 16,500, Castory Mwinuka mkazi wa Mwanza aliyechangia sh 30,000 na mwingine aliyekataa kutajwa jina lake aliyechangia sh 50,000.
Hamad, mwenye umri wa miaka minne sasa, wamezaliwa wawili akiwa na dada yake, Rehema anayesoma darasa la kwanza huku akienda shule kwa kusuasua.
Mtoto huyu mwenye upeo wa hali ya juu, aliweza kueleza maswahiba anayokutana nayo katika kazi yake ya kuokota chupa za maji.
“Huwa naamka asubuhi mama na baba wakiwa wanaenda shamba, mimi naenda kuokota chupa, natembea jalalani, barabarani na kama hapa (Esperanto) naokota, zikijaa nazipeleka nyumbani na mama akirudi shamba anaziuza,” alinukuliwa Hamadi katika makala hiyo.
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment