MAUAJI ya kikatili yameibuka tena mkoani Geita baada ya watu wasiojulikana kuvamia maeneo matatu usiku wa Aprili 27 na kuwaua kwa kuwachinja na kutenganisha viungo vyao watu watatu kwa imani za kishirikina.
Tukio la kwanza la mauaji hayo limetokea katika Kitongoji cha Chemamba, Kijiji cha Chikobe, Kata ya Nyachiluluma ambapo Joyce Matalama (70) alichinjwa na kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiofahamika.
Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Kazimili Malindi, alisema kuwa Aprili 27 mwaka huu alipata taarifa za tukio hilo, na kwamba bibi huyo aliyekuwa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji na ndugu yake, aliuawa na watu hao akiwa njiani kurejea nyumbani kwake katika uwanja wa shule.
Mtendaji huyo alisema hadi sasa watu wawili wanashikiliwa kutokana na tuhuma za mauaji, akiwemo mtoto wa marehemu waliyekuwa naye kwenye kilabu hicho, Daniel Samsoni pamoja na kiongozi wa sungusungu, Emmanuel Enos.
Tukio la pili limetokea katika Kijiji cha Itale, Kata ya Katoma ambapo Mariam Kapalata (67) aliuawa kwa mtindo huo huo na watu wasiofahamika, waliovamia nyumbani kwake majira ya saa moja na nusu usiku.
Diwani wa Kata ya Katoma, Angelo Komanya, alisema tukio hilo ni la pili katika kata hiyo tangu kuanza kwa mwaka huu, na la nne katika kata yake.
Mauaji mengine alisema yametokea katika Kijiji cha Mharamba.
Katika tukio la tatu, Kabula Yohana (60) aliuawa kwa kuchinjwa na kutenganishwa kichwa na watu wasiofahamika katika Kijiji cha Kagu na kutokomea usiku wa siku hiyo.
Diwani wa Kagu, Nkukura Lukondo, alisema Aprili 27, mwaka huu majira ya saa 2 usiku, watu wasiofahamika walimvamia bibi huyo akiwa amelala nyumbani kwake na kutenganisha viungo vyake.
Diwani Lukondo alisema hilo ni tukio la nne katika kata yake tangu mwaka jana, na ambayo yanasukumwa na imani za kishirikina, na ameitaka jamii kuachana na imani hizo na kwamba kuna kundi la watu wanaowafadhili wauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Joseph Konyo, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo, na kwamba watu kadhaa wamekamatwa na wameanzisha uchunguzi mkali juu ya matukio hayo.
No comments:
Post a Comment