Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani juzi aliwasilisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15, huku ukumbi wa Bunge ukiwa na wabunge 14 tu, wakiwemo mawaziri watano.
Kutokana na hali hiyo waziri huyo alionekana kama anawasilisha bajeti ya wizara yake mbele ya viti vitupu vilivyopo katika ukumbi huo. Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 355, wakiwemo mawaziri na naibu mawaziri 55.
Vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea mjini hapa huanza saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana na kuendelea tena kuanzia saa 11 jioni hadi saa mbili usiku. Kombani aliwasilisha bajeti hiyo saa 10 jioni ambapo mpaka anamaliza kuisoma saa 11 jioni, idadi ya wabunge waliokuwepo katika ukumbi huo ilifikia 87, huku wakiongezeka mawaziri sita tu na kufanya idadi yao kufikia 11.
Mpaka inafika saa 10:15 jioni idadi ya wabunge iliongezeka na kufikia 24 wakiwemo mawaziri hao, dakika 20 baadaye idadi yao iliongezeka tena na kufikia wabunge 38.
Licha ya uchache wao baadhi yao walikuwa hawatulii eneo moja, kwani walikuwa wakihama hama huku wakionekana kujadiliana jambo na wenzao.
Mpaka Kombani anamaliza kuwasilisha bajeti yake, saa 11:05 idadi ya wabunge waliokuwa katika ukumbi huo ilifikia 87, wakiwamo mawaziri hao.
Pamoja na uchache huo bajeti ya wizara hiyo ilipitishwa juzi hiyo hiyo licha ya mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde kumtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuzingatia akidi ya wabunge kwa madai kuwa ni ndogo kupitisha bajeti hiyo.
Hata hivyo, Spika Makinda alisema akidi hiyo siyo tatizo na kusisitiza kuwa huwa inazingatiwa zaidi wakati wa kupitisha bajeti kuu kwa maelezo kuwa kila mjumbe huitwa kwa jina lake katika upitishwaji huo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu utoro wa wabunge Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alisema kuwa akidi ya wabunge huzingatiwa zaidi kama kutakuwa na kikao cha kutoa uamuzi.
“Kama kuna kikao cha kutoa uamuzi ni lazima tuangalie akidi lakini kama ni vikao vya kawaida hukuna tatizo lolote” alisema
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment