Monday, 12 May 2014
DODOMA WAPAMBANA NA IMANI ZA KISHIRIKINA
KUTOKANA na imani potofu iliyojichimbia miongoni mwa jamii, mwaka jana, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, alikumbwa na zomeazomea ya wananchi wa wilaya hiyo akichukua hatua muhimu sana ya kupiga marufuku waganga wa kutoa uchawi kufanya kazi zao ndani ya wilaya hiyo.
Wananchi hao walikuwa wakitaka waganga hao waruhusiwe kufanya kazi ya kutoa uchawi ndani ya wilaya hiyo huku DC huyo akiwa hakubaliani na maamuzi hayo.
Haikuwa kazi rahisi kwani kundi kubwa la wananchi walikuwa hawataki kusikia waganga hao wakipigwa ‘stop’ kufanya kazi ndani ya wilaya hiyo, kwani walikuwa tayari kuchanga kiasi chochote cha fedha kuhakikisha waganga hao wanafanya kazi ya kufichua wachawi, jambo ambalo kama lingeruhusiwa lingeleta uhasama mkubwa miongoni mwa wananchi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, kamwe asingekubali kubadilisha uamuzi huo, hivyo akawataka wananchi waachane na mambo ya kishirikina na wafanye shughuli za maendeleo.
Kwa muda mrefu Dodoma ulikuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo ilivamiwa na waganga wa kutoa uchawi maarufu kama lambalamba lakini tatizo hilo linaonekana kupungua kama sio kuisha kabisa kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuhakikisha waganga hao matapeli wanaondoka.
Juhudi hizo zilikuwa ni pamoja na kuelimisha wananchi ili kuweza kuachana na imani potofu. Pia kuna juhudi zilizofanywa na Mkuu wa Mkoa na wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma ili kufukuza waganga hao, juhudi ambazo mara kadhaa zilikuwa zikigonga ukuta kutokana na wananchi kutaka waganga hao watatue shida zao ambazo kimsingi hazitatuki zaidi ya kutapeliwa.
Katika maeneo ya Gawaye na Chihanga, Manispaa ya Dodoma, wananchi walikuwa wakishindwa kwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali na kupanga foleni kwa waganga kwa lengo la kutatuliwa matatizo yao. Hilo pia lilisababisha kuzorota kwa uchumi kwenye ngazi ya kaya.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi anasema waganga hao hawastahili kuwemo katika jamii kwani wamekuwa wakitapeli wananchi fedha zao kwa madai ya kutoa uchawi huku wakifanya unyanyasaji mkubwa wa kijinsia kwa wanawake, mbali na kuchonganisha jamii.
Anasema licha ya waganga hao wadanganyifu kupita kila kaya kukusanya fedha za kutoa uchawi pia kila kijiji walichokuwa wakipita walikuwa wakichagua wanawake wa kuwapikia na hata kulala nao. Dk Nchimbi anasema aliwahi kupata malalamiko kuwa katika baadhi ya vijiji, lambalamba hao kabla ya kuingia ndani lazima kuwe na wanawake waliovua nguo walale mlangoni ambapo huwaruka kisha kuingia ndani.
Akasema huo ni udhalilishaji mkubwa kwa wanawake ambao jamii inatakiwa kukemea vitendo hivyo kwa nguvu zote. Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally, anasema lambalamba hao walikuwa wakitumia uelewa mdogo walionao wananchi ili kuwarubuni kwa viini macho na kisha kuwatapeli pesa lakini wakiacha nyuma uhasama na jamii iliyosambaratika.
Anasema miongoni mwa wilaya zilizoathirika na tatizo la lambalamba katika mkoa wa Dodoma ni Chamwino kutokana na baadhi ya viongozi wa vijiji kuwaruhusu waganga hao kufanya shughul zao za kitapeli katika maeneo yao. Hata hivyo, anasema juhudi za serikali kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi zilifanikisha kuwaondoa waganga hao ndani ya wilaya hiyo.
Godfrey Wambali, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Kati Dodoma, anasema kuna sheria inayozungumzia vitendo vya uchawi. Wambali anasema Sheria ya uchawi (Witch craft Act ) namba 12 ya mwaka 1998, kwenye kifungu cha 3 kinaongelea vitendo hivyo kuwa ni kosa la jinai.
Anasema mtu yeyote akitumia kauli yake ama vitendo na kujifanya ana nguvu za uchawi, anayefanya, anayetumia au kujifanya ana vifaa vya uchawi, kusambaza kwa watu wengine kushawishi watu wengine kujiunga na uchawi na kutishia kutumia uchawi, wote wanakuwa wamefanya makosa chini ya kifungu hicho cha sheria.
Pia anasema kifungu cha 5 cha sheria hiyo kinaongelea adhabu ambapo mtu yeyote anayetenda vitendo vilivyotajwa katika sheria hiyo na kusababisha kifo, ugonjwa, majeraha, msiba au balaa lolote katika jamii au jumuiya ya watu fulani kwa mtu pekee mnyama au kusababisha uharibifu wa mali yoyote atakumbwa na adhabu ya kifungo isiyopungua miaka saba.
Mwanasheria huyo anasema mtu ambaye anafanya makosa yaliyopo ndani ya sheria hiyo pasipo kujua, adhabu yake ni faini ya Sh 100,000 au kifungo kisichopungua miaka mitano. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime anasema lambalamba lilikuwa ni tatizo kubwa katika Mkoa wa Dodoma ambapo watu kadhaa walikamatwa wakijihusisha na vitendo hivyo.
Misime anasema watu hao walikuwa wakijihusisha na vitendo vya kishirikina kwa kujifanya wanaagua na kufichua wachawi katika vijiji mbalimbali. Akitoa mfano anasema Aprili 16, mwaka 2013 katika kijiji cha Mbalawala, Manispaa ya Dodoma waliweza kukamata lambalamba sita ambapo waganga ambao walidai kufichua wachawi wanaozuia mvua zisinyeshe katika maeneo mbalimbali ya mkoani Dodoma.
Anasema baadhi ya waganga waliokamatwa walikuwa wakitoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam. Anazitaja mbinu walizokuwa wakitumia watu hao ni pamoja na kuwaita watu wachawi na kuchukuliwa fedha zao kwa nguvu. Anataka wananchi kuacha kushabikia vitendo hivyo kwani ni njia iliyobuniwa na baadhi ya watu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kudhalilisha na kujenga chuki ndani ya jamii kutokana na kuwaita wengine wachawi.
Anafafanua kuwa kupitia mradi huo batili, waganga hao matapeli wamekuwa wakijipatia fedha taslimu, kuku, ng’ombe, mbuzi na hata nafaka. Anasema jambo la kushangaza ni kwa kuna baadhi ya viongozi na wasomi wanashaabikia shughuli zinazoendeshwa na watu hao.
Mwenyekiti Chama cha Waganga wa Tiba za Asili na Wakunga wa Jadi (Chawatiata) Mkoa wa Dodoma, Issa Mohamed Mdoe, anasema chama kinawatambua waganga wa kutoa uchawi maarufu kama lambalamba kuwa ni wahuni. “Lambalamba ni vijana wasio na kazi maalumu ambao wameunda kikundi na kujifanya ni waganga na hivyo kuwapa usumbufu wananchi na kujifanya wanatoa uchawi,” anasema.
Pia anasema chama kimekuwa kikifanya juhudi mbalimbali kuhakikisha uhuni huo unakoma ikiwemo kupita kata kwa kata na vijiji kuelimisha wananchi wasikubali kurubuniwa na kuchukuliwa fedha zao kwa madai kuwa watatolewa uchawi na kwamba huo ni utapeli kwani hakuna uchawi unaotolewa.
“Vitu wanatega wenyewe, wanakwenda usiku na kuvichimbia halafu asubuhi wanasema wamekuta nyumba fulani ina uchawi,” anasema. Anabainisha kuwa tatizo la lambalamba zaidi lilikuwa katika kata ya Msamalo, Sagala, Buigiri na Chilonwa zilizopo wilaya ya Chamwino.
Akitoa mfano anasema katika eneo la Chilonwa iliwahi kutokea rabsha ambapo lambalamba waliingia ndani ya nyumba ya mtu na mwenye nyumba akaamua kupiga risasi ambayo ilimpata pajani mmoja wa lambalamba hao lakini kwa bahati hakupoteza maisha. Anasema Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally alishirikiana na chama hicho pamoja na viongozi wa kata kuhakikisha lambalmba hawaingii tena Chamwino.
Mdoe anasema lambalamba hao wanapofika kwenye vijiji husika wamekuwa wakisema wana vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo, lakini wanapotakiwa kuonesha vibali hivyo wamekuwa wakikimbia.
“Chawatiata inasikitika kwa sababu baadhi ya viongozi wa vijiji na kata walikuwa wakishirikiana na lambalamba kwa kupewa fedha kidogo na kuruhusu wafanye shughuli zao, jambo ambalo ni uvunjifu wa amani kwani hakuna mtu mwenye haki ya kuingia eneo la mtu mwingine bila ridhaa yake,” anasema.
Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma, Audry Njelekela, anasema zipo changamoto za kupambana na VVU na ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Dodoma.
Anasema amewahi kusikia tatizo la waganga wa kutoa uchawi kutumia wembe mmoja kunyoa zaidi ya watu watatu kitu ambacho kinahatarisha afya kwani wengi wanaonyolewa vipara vya wembe wamekuwa wakiumia hata kutoka damu na wembe huo unapotumiwa na mtu mwingine ni rahisi kuambukizana magonjwa kama mmoja wao ameathirika na virusi vya Ukimwi. Anataka wananchi kuachana na imani za kishirikina ili wawe salama.
“Elimu zaidi inahitajika ili wananchi waweze kuelimika na kuachana na imani hizo ambazo nyingi zina madhara,” anasema. Ally Biringi ni chifu wa Wagogo na mkazi wa Makulu Dodoma. Yeye anasema kazi ya lambalamba haiwezi kukubalika katika eneo lolote kwani waganga hao ni matapeli ambapo wakati mwingine wamekuwa wakitaja mtu au watu wanaozuia mvua, zamani mambo haya hayakuwepo kabisa.
“Leo lambalamba ana uwezo wa kuingia nyumbani kwa watu anadai anatoa uchawi kisha anataka hela, hapo wananchi wanaona kama wanasaidiwa kumbe wanatapeliwa,” anasema.
Kulingana na mzee huyo ni muhimu wananchi wakaendelea kuwakataa watu wa namna hiyo wanapofika katika maeneo yao kwani ni matapeli wenye lengo la kuchonganisha watu na kuleta uhasama mkubwa mbele ya jamii. Makala haya yameandikwa kwa uwezeshwaji wa Tanzania Media Fund.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment