VIJANA wanne wakazi wa mji wa O’murushaka, Kata ya Bugene, wilayani Karagwe, wanaishi kwenye vyoo vya huduma vya wasafiri vilivyopo katika mji huo kwa miezi sita sasa kwa madai ya ugumu wa maisha.
Vijana hao walikutwa wamelala katika vyoo hivyo juzi wakati abiria walipotaka kujisaidia ili kujiandaa na safari zao.
Mmoja wa vijana hao, Bosco Venance (30), alisema shughuli zao kwenye eneo hilo ni kubeba mizigo na wamelazimika kuweka makazi kwenye vyoo kutokana na ugumu wa maisha.
Venance alisema kipato wanachopata ni kidogo, hivyo hawawezi kupanga nyumba na kununua chakula, ndiyo maana wamelazimika kuishi kwenye vyoo ili kukabiliana na ugumu wa maisha.
“Tumeishi kwenye choo hiki zaidi ya miezi sita sasa. Vyumba vya mji huu ni kati ya sh 15,000 hadi 20,000 unavyoona hali hii na wingi wa magari, wakiwemo wapiga debe hizo pesa tutazipata wapi?” alihoji Venance.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo, Vegirance Kahungya, alikiri vijana hao kutumia vyoo hivyo kama makazi yao.
Alisema ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa kata, wamekuwa wakiwafukuza, lakini baada ya muda wanarudi.
Kahungya alisema ingawa kuna kufuri, vijana hao hutumia funguo bandia na wakati mwingine kutumia nguvu kuvunja milango hiyo.
Msimamizi wa vyoo hivyo, Jonestha Kanyiginya, alisema vijana wanaoishi kwenye vyoo hivyo wamekuwa kero katika utendaji wa kazi, kwani usiku vyoo hivyo hugeuzwa kuwa makazi, hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji.
Alitaja changamoto nyingine anazokabiliana nazo kuwa ni baadhi ya vijana katika mji huo kujihusisha na vitendo vya uporaji na uvutaji bangi.
Aliuomba uongozi wa kata kutoa ulinzi ili wanaotumia vyoo hivyo kama makazi, wachukuliwe hatua.
1 comment:
15:36
1
Emungu uwasaidie wana karagwe.
Post a Comment