PICHA HAIHUSIANI NA HABARI HUSIKA...
DIWANI wa Shume, Rashird Kisimbo, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwafungulia mashitaka ya mauaji askari wake sita wa Kituo cha Polisi Lushoto wanaotuhumiwa kumuua raia mmoja na kujeruhi mwingine.
Askari hao wanatuhumiwa kumuua kwa risasi, mkazi wa Kijiji cha Viti, wilayani hapa, Hamis Seif (25) na kumjeruhi Athuman Mgazija wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.
Chanzo cha mauaji hayo ni hatua ya askari hao kuvamia nyumba ya Mohamed Hamis, saa tano usiku wakidai kutekeleza amri ya Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kwa kile walichodai mwananchi huyo alipuuza wito wa mahakama hiyo katika shauri la madai.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za uchunguzi wilayani hapa kwa wiki mbili, umebaini tikio hilo lilitokea Oktoba 17 mwaka jana, lakini hadi sasa limefanywa siri na mamlaka husika, ikiwamo kushindwa kuwawajibisha askari waliohusika na mauaji hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, diwani huyo alihoji ukimya wa Jeshi la Polisi kutowakamata askari hao huku wakihamishiwa vituo nje ya Wilaya ya Lushoto.
Diwani huyo aliungana na wananchi hao kukanusha madai ya askari hao kuwa waliowavamia na kuwashambulia walikuwa ni majambazi, na kusema askari hao walivamia nyumba ya mwananchi huyo bila kushirikisha uongozi wa ngazi zote kuanzia kitongoji, kijiji hadi kata.
Alisema kuwahamisha vituo na kuwashusha vyeo askari hao si suluhisho na hakuondoi uhalisia wa tukio hilo, huku akitupia lawama uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Lushoto kwa kutoingilia kati tukio hilo
TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment