Ujumbe wa Tanzania katika mikutano muhimu inayofanyika Marekani wameipigia debe nchi yao wakitaka ikumbukwe.
Katika mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UN) na mkutano wa wazi wa tisa wa kikosi kazi kuhusu mapendekezo ya ajenda za malengo mpya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 (SDGs), wamekuwa wakitetea masilahi ya nchi kwa kushiriki na kuchangia majadiliano ya mada mbalimbali zinazohusiana na mikutano hiyo.
Akichangia katika mada iliyohusu Technolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa alisema mwaka hadi mwaka Tanzania na Afrika imeendelea kupiga hatua katika teknolojia ya habari na mawasiliano licha ya changamoto mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kutokuwapo kwa uratibu kati ya wazalishaji wa takwimu za ICT na watumiaji na kati ya wazalishaji na watoaji wa takwimu ambao ni chanzo muhimu cha taarifa.
Alisema tatizo hili kama halitarekebishwa, linaweza kusababisha uchapishaji usio sahihi wa takwimu kuhusu ICT, jambo ambalo linaweza kusababisha utoaji uamuzi wenye makosa.
Alisema uboreshaji na uratibu kati ya wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa takwimu, utaepusha kujirudia kwa makosa yakiwamo ya matumizi ya rasilimali fedha na watu, rasilimali ambazo ni haba katika Afrika.
‘’Kipengele cha takwimu za ICT kinapaswa kuingizwa katika mikakati ya kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya takwimu na katika mipango ya kazi ya kikanda, ’’ alisema.
Dk. Chuwa alisema ukusanywaji wa takwimu katika ngazi za kitaifa lazima uimarishwe kwa kuweka utaratibu kati ya taasisi husika pamoja na Ofisi za Taifa za Takwimu.
Kuhusu uwezeshaji, alisema Afrika inahitaji kuimarisha uwezo wake wa kutafuta rasilimali ndani ya Afrika ili hatimaye Afrika ijijengee uwezo wa kuboresha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa viashiria vya msingi vya ICT katika Afrika.
Alisema Tanzania ingependa kuona wataalamu walioandaa mfumo huo, wanakuja na mkakati wa utoaji mafunzo na uwezeshaji kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania
No comments:
Post a Comment