.
Raia wa China, Huang Gin, Xu Fujie na Chen Jinzha wamedaiwa kutoa hongo ya Sh30.2 milioni kwa polisi na askari wa wanyama pori ili wasipekue nyumba waliyokuwa wakiishi iliyo Mtaa wa Kifaru Mikocheni.
Washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,880 vyote vikiwa na thamani ya Sh5.4 bilioni.
Shahidi wa upande wa mashtaka, ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana na amri ya Hakimu Isaya Arufani wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu iliyotolewa jana ya kuvitaka vyombo ya habari kutotaja majina ya mashahidi watakaotoa ushahidi kwenye kesi hiyo, alidai kushuhudia tukio hilo.
Alidai kuwa wakati wakiendelea kufanya upekuzi kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi washtakiwa hao, Huang Gin alivuta droo na kutoa bahasha iliyokuwa na fedha ndani ambazo walipozihesabu zilikuwa ni Sh30.2 milioni kama kishawishi cha kuwataka wasiendee kuipekua nyumba hiyo.
“Hatukukubaliana na ofa hiyo kwa sababu tuliamini kuna kitu ndani yake na ni lazima tufanye upekuzi na kiasi hicho cha fedha tukakichukua kama kielelezo cha ushahidi,” alidai shahidi huyo.
No comments:
Post a Comment