Mdomo ni kiungo kinachopewa nafasi kubwa katika urembo wa mwanamke kutokana na kuwa ni miongoni mwa viungo vinavyoonekana kwa haraka zaidi.
Wengi wamekuwa wakiweka vipodozi mbalimbali kwenye midomo yao kama vile rangi ya mdomo (lipstick, lipbam), wanja na kadhalika, lengo likiwa ni kuifanya iwe na mvuto.
Licha ya vipodozi vyote na rangi na aina mbalimbali ambazo wengi hupaka katika midomo yao, ukweli utabaki kwamba, hakuna mwanamke asiyependa midomo yake kuwa na rangi ya pinki.
Lakini, kutokana na sababu za hapa na pale, wapo ambao hujikuta wakiwa na weusi kwenye midomo, hali inayowafanya wengi kuhangaika kutafuta tiba ya tatizo hilo.
Zipo sababu mbalimbali zinazochangia kutokea kwa hali hii, zikiwemo uvutaji wa sigara, kupigwa na miale ya jua kwa muda mrefu, unywaji wa kahawa kupita kiasi pamoja na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali.
Leo tutaangalia njia mbalimbali za asili zinazoweza kutumika kuondoa weusi na kuiacha midomo ikiwa na mvuto wa hali ya juu.
Miongoni mwa njia hizo ni matumizi ya limao na asali. Mchanganyiko wa limao na asali husaidia kwa kiasi kikubwa kutoa taka ngumu ambazo hung’ang’ania kwenye ‘lips’ na kuziacha zikiwa na mng’ao wa asili.
Chukua mchanganyiko huo kisha paka kwenye midomo yako na kaa nao kwa muda usiopungua nusu saa, kisha futa kwa kitambaa kisafi. Fanya hivyo mara mbili au tatu kwa siku kwa matokeo mazuri.
Njia nyingine ni unywaji wa juisi ya tango, mtu anayependelea kunywa juisi ya tango kila siku ana uhakika wa kung’arisha ‘lips’ zake na kuzifanya kuwa na rangi ya pinki.
Maji pia ni tiba tosha ya kuifanya midomo kuwa na rangi nzuri yenye mvuto na mng’aro wa asili.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward
No comments:
Post a Comment