Wapo wanawake wenye ushawishi mkubwa katika jamii. Wengi wa wanawake hawa, wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kuhakikisha wanabadilisha maisha ya mwanamke wa Kitanzania.
Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuleta maendeleo kwa watu wote, kwani ni ukweli usiopingika kuwa unapomkomboa mwanamke mmoja, unakuwa umekomboa jamii.
Sofia Mwakagenda ni miongoni mwa wanawake hao wachache waliofanya kazi kubwa ya kuwawezesha wenzao kiuchumi.
Mama huyo ni Mkurugenzi wa Asasi ya Tanzania Women and Youth Development Society (TWYDS), amekuwa akitumia muda mwingi kubuni miradi mbalimbali yenye lengo la kuwezesha kundi hilo muhimu katika jamii ya Kitanzania.
Je, ni kwa nini aliamua kujikita katika uwezeshaji wa wanawake?
Sofia anabainisha sababu ya kwanza kwamba ni yeye kuwa mwanamke. “Kimsingi mwanamke ni mlezi na mjenzi wa familia na jamii kwa jumla,”anasema.
Anaongeza: “Hivyo, ili jamii iendelee na kujengeka kwa ufanisi, nguvu ya mwanamke inahitajika. Kwa kuwa nina uwezo wa kuwaleta pamoja wanawake wengi niliona ipo haja ya kubuni miradi inayowalenga, ili kutimiza lengo langu.”
Mwakagenda anasema kuwa, awali wanawake walionekana ni watu tegemezi, wasiojitambua wala kuweza kuamua mambo yao, hata yale ya ndani mpaka kuwepo kwa msaada wa watu fulani.
Anabainisha kuwa kwa sasa mambo yamekuwa tofauti, kwani tangu kuanzishwa kwa miradi ya uwezeshwaji kwa ajili yao, wanawake wamepiga hatua katika nyanja tofauti.
TWYDS imewafikia wanawake wangapi?
Sofia anaeleza kuwa asasi ya TYWDS inafanya kazi katika mikoa saba nchini, ikitoa kipaumbele kwa wanawake na vijana.
Anafafanua kuwa mbali na Dar es Salaam, mikoa iliyofikiwa na asasi hiyo ni pamoja na Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa, Arusha, ambapo miradi mbalimbali imeshafanyika ikiwamo ya sasa uwezeshwaji wa wanawake wilayani Temeke ambapo uliwafikia wanawake 300
No comments:
Post a Comment