Mjumbe wa Bunge la Katiba, Makeresia Pawa ametaka Rasimu ya Katiba mpya iliyowasilishwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ifumuliwe vinginevyo yupo tayari kurudi kijijini kwake Mbeya.
Mjumbe huyo anayewakilisha Vyama vya Wafugaji akizungumza kwa hisia kali kwenye semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Utetezi wa Haki za Wakulima na Wafugaji kwenye matumizi ya ardhi katika Katiba, anasema rasimu hiyo kama ilivyo haiwezi kuingizwa matakwa ya wafugaji, wakulima au wavuvi katika ardhi kwa sababu Jamhuri ya Muungano haina ardhi.
“Nilipopata rasimu na kuisoma nilijiuliza jinsi mkulima, mfugaji atakavyoingiza masuala ya haki zake kwenye katiba hii ambayo ni ardhi wakati mamlaka husika kiuhalisia haitakuwa na ardhi,” anaeleza.
Anasema kwa msingi huo kama siyo wa kwanza, alikuwa wa pili kutaka rasimu hiyo ifumuliwe ili uwakilishi wake ulete maana bungeni.
Pawa alisema kinyume na hivyo, yupo tayari kurejea kijijini ili asubiri rasimu itakayokuwa inawahusu wakulima na wafungaji, akieleza kuwa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba inahusu masuala ya uongozi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Dodoma, Pawa anajibu maswali kama ifuatavyo;
Mwananchi: Kwanini uliomba nafasi ya kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge maalumu?
Pawa: Niliomba kuwawakilisha wafugaji kuhakikisha haki zao zinaingizwa katika Katiba, hususan umiliki ardhi.
Mwananchi: Bila shaka kabla ya kuomba uwakilishi ulisoma vizuri rasimu hii na kuielewa. Nini kimebadilika mpaka ufikie uamuzi wa kuwa na msimamo wa kutaka ifumuliwe na kubadilishwa muundo wake ndipo uijadili?
Pawa: Tatizo kubwa linalowakabili wafugaji, wakulima na hata wavuvi ni umiliki na matumizi ya ardhi. Tutaliweka vipi kwenye Katiba ambayo inahusu mambo Saba ya Muungano tu? Ndiyo maana nataka ifumuliwe, iwekwe kwenye muundo ambao unabeba mambo mengi zaidi likiwamo la ardhi.
Mwananchi: Kwa kuwa uliisoma na kuielewa kabla hujaomba, hukutambua kuwa haikuhusu kama unavyodai?
Pawa: Hilo nililiona lakini nikaamua niombe tu ili nikichaguliwa nije kulisema hapa na ndilo ninalofanya sasa hivi. Hii rasimu isipofumuliwa tutatengeneza taifa la tatu lisilo na ardhi wala watu, litakuwa taifa la wateule
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment