Jeshi la polisi mkoani Dar es salaam limefanikiwa kuwakamata watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi baada ya kulazimika kutumia risasi za moto kuwadhibiti watu hao,waliokuwa wakisafirisha silaha kutoka mkoani Kigoma kupitia Tabora kwenda jijini Dar es salaam kwa nia ya kutekeleza matukio ya kihalifu.
Tukio hilo limevuta hisia za watu wengi katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo jijini dar es salaam baada ya jeshi la polisi kupata taarifa kutoka kwa samaria wema na kuweka mtego na kisha kufanikiwa kuwakamata watu hao wawili wakiwa na bunduki moja aina ya smg yenye magazine mbili pamoja na risasi 148.
Mara baada ya askari kanzu kutoka makao makuu ya jeshi la polisi kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi ITV imezungumza na watuhumiwa ambao wamedai kuinunua bunduki hiyo wilayani Kasulu mkoani Kigoma kutoka kwa raia wa Burundi kwa kiasi cha shilingi milioni 1.5 ili waje na kwamba waliagizwa kuileta Dar es salaam kwa malipo ya shilingi milioni 2 ili itumike katika matukio ya kijangili.
Nao baadhi ya wananchi waliokuwepo katika eneo la tukio wamelipongeza jeshi la polisi na kulitaka kuongeza kasi ili kujenga imani ya jeshi hilo kwa wananchi kutokana na imani iliyoanza kujengeka ya baadhi ya polisi kushirikiana na majambazi na kushauri pia kuimarishwa kwa ukaguzi katika vizuizi vya barabarani.
Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam limethibitisha kukamatwa kwa watu hao na kwamba mahojiano yanafanyika ili kupata taarifa za kina kutoka kwa watu hao zitakazowezesha kuuvunja mtandao wao
CHANZO: IPP
No comments:
Post a Comment