Hebu fikiri... Unaamka asubuhi na kukuta kundi la majirani nje ya mlango wa nyumba yako. Uwepo wao siyo kwa lengo la kukusalimu, bali kukupa ujumbe wa hatima ya maisha yako.
Hali hii ndiyo iliyomkuta Veronica Kibuga (85) mkazi wa Kitongoji cha Kahangala wilayani Magu, Mwanza ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa akiishi kwa hofu kwani anasubiri utekelezaji wa ‘adhabu ya kifo’ kukatwa kwa mapanga kutokana na tuhuma kuwa yeye ni mchawi.
Ujumbe uliotumwa kwake uliandikwa kwa lugha ya Kisukuma na ulikutwa kisimani ambako waliupeleka walipokwenda kuteka maji na unasema: “Bamayo yashikaga izamu igawo ya kukatwa mapanga”, ukimaanisha: ‘Imefika zamu yako ya kukatwa mapanga’.
Majirani wamejaa nje ya nyumba ya Kibuga kwani wanafahamu fika kwamba mwandishi wa ujumbe ule hatanii, kwani wote waliowahi kupata ujumbe kama wake waliuawa. Huyu ni mmoja, lakini ukweli ni kwamba wanawake wengi, hasa wazee wanaishi na makovu na wengine wamepoteza maisha baada ya kupokea taarifa kama hizi.
Wakati dunia nzima ikisherekea Siku ya Mwanamke Duniani leo hii, wanawake wa aina ya Kibuga wako ndani wamejifungia wakihofu usalama wao kutokana na kuishi katika jamii ambayo inamwona kama mkosi na chanzo cha matatizo yote.
Wanawake wanasherehekea leo na kutukuzwa kwa mchango wao mkubwa katika masuala mbalimbali, lakini wapo wanaohitaji ukombozi ili watoke kwenye madhila ambayo yamewafanya kuishi kwa wasiwasi mkubwa.
Hata watoto wadogo wanapofariki, huwa inaaminika kuwa mwanamke mchawi ndiye ‘aliyemla nyama’. Dhana hii imewafanya baadhi ya wanaume vijijini kuwaachia wanawake kazi ya kuchimba makaburi.
Haya ndiyo yaliyomkuta Kibuga ambaye leo hii anatembea na waraka wa kifo mkononi, akisubiri ‘siku ya hukumu yake’.
Simulizi yake
Kabugu anasema: “Siku moja niliamka asubuhi na kukuta majirani zangu wakiwa nje ya nyumba yangu, walikuwa wameniletea ujumbe wa kifo kutoka kwa mtu asiyejulikana akisema ataniua mimi na watoto wangu kwa kuwa ni wachawi.”
Barua hiyo iliyotumwa na mtu anayejiita ‘Meneja wa Kujiajiri’ ilieleza kuwa Januari 30 atafika katika nyumba ya bibi huyo na kummaliza kwa kumkata mapanga yeye na familia yake.
Watoto wa Veronica ambao ni Usia na Magdalena Kibuga nao wametajwa kuwa watauawa pamoja na mama yao kwa kuwa wanasaidiana naye katika masuala ya uchawi.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment