Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Saleh Jidawi Akifungua Warsha ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Wizara ya Afya na Mangariba juu ya Kutahiri watoto wa kiume ili kuepukana na Ugonjwa wa Fistula.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Interplast ya nchini Uholanzi Dkt. Rein Zeeman aliyesimama mbele akiendesha Warsha ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Wizara ya Afya na Mangariba juu ya Kutahiri watoto wa kiume ili kuepukana na Ugonjwa wa Fistula.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Interplast ya nchini Uholanzi Dkt. Rein Zeeman kushoto akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya Waandishi wa habari juu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Wizara ya Afya na Mangariba juu ya Kutahiri watoto wa kiume ili kuepukana na Ugonjwa wa Fistula Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Saleh Jidawi katika picha ya pamoja na Wanachama wa Taasisi ya Interplast baada ya Ufunguzi wa Warsha ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Wizara ya Afya na Mangariba juu ya Kutahiri watoto wa kiume ili kuepukana na Ugonjwa wa Fistula.
Na Faki Mjaka- Maelezo Zanzibar 06/03/2014
Taaluma ndogo katika kutahiri Watoto wa kiume imeelezwa kuwa ni miongoni mwa Vyanzo vya Ugonjwa wa Fistula ambapo Watoto waliotahiriwa huwa na njia zaidi ya moja ya kupitishia Mkojo.
Hali hiyo imepelekea Taasisi ya Interplast ya nchini Uholanzi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuandaa Warsha ili kukabiliana na tatizo hilo kwa Watoto wa Zanzibar.
Akizungumza katika uzinduzi wa Warsha hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Saleh Jidawi amesema ni vyema Mangariba wakapatiwa mafunzo kutoka kwa Wataalam ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Amesema kupatikana kwa taaluma ya kutosha kutalifanya tatizo hilo kupungua na kupelekea Afya za watoto kuimarika.
“Sisi Serikali kazi yetu ni kuhakikisha Wananchi wanaondokana na Matatizo ndio maana tukashirikiana na Taasisi hii ya Interplast ili kuwajengea uwezo Mangariba wetu juu ya tatizo la Fistula” alisema Dkt. Jidawi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Interplast Dkt. Rein Zeeman amesema wamekuja Zanzibar kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri ili Mangariba waweze kupata mbinu bora za kufanya kazi zao.
Amefahamisha kuwa Jamii inapaswa kuelewa kwamba kazi ya Kutahiri inahitaji kufanywa kwa taaluma na tahadhari kubwa kama inayochukuliwa katika Upasuaji wa binadamu.
“Jamii inapaswa kujua kuwa Kutahiri ni jambo la hatari na hivyo linapaswa kufanywa tu na watu waliopatiwa mafunzo ya kutosha” Alisisitiza Dkt. Zeeman.
Naye Mshauri wa Taasisi ya Interplast Bi. Ruth Lester amesifia mashirikiano ya kutosha wanayoyapata kutoka kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.
Ameongeza kuwa matarajio yao nikuona kazi ya Ungariba haifanywi na kila mtu badala yake ifanywe na Wataalam waliosajiliwa ili kuepukana na Tatizo la Fistula kwa Watoto.
Amesema utafiti waliofanya wamegundua kuwa kila Watoto 1,000 Wakiume waliotahiriwa Zanzibar wawili hadi watatu wamepata tatizo la Vistula kutokana na kutahiriwa vibaya.
“Tumefanya utafiti katika sehemu mbali mbali duniani kuhusu kutahiri,kwa mfano Mji wa Birmingham Watoto 50,000 waliotahiriwa hakuna aliyegundulika na tatizo lakini kwa Zanzibar kila Watoto 1,000 Wawili hadi watatu wamepata tatizo” Aliongeza Dkt.
Semina hiyo ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Afya na Mangariba imefanyika Ukumbi wa Hoteli ya Ocean View mjini Unguja ambapo pia itaendelea katika Kisiwa cha Pemba ili kuondokana na ugonjwa wa Fistula kwa Watoto Zanzibar.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment