Monday, 6 January 2014

SITA WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA BOTI YA MV KILIMANJARO



WATU sita wamefariki dunia na wengine watatu kuokolewa katika boti ya abiria ya MV Kilimanjaro iliyokumbwa na dhoruba ya mawimbi makali kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa baharini.
Ajali hiyo ilitokea jana katika eneo la mkondo wa Nungwi wakati boti hiyo ikitoka Pemba kurudi Unguja.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo watoto watatu wamefariki dunia pamoja na wanawake watatu wenye umri kati ya miaka 36-50.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alithibitisha ajali hiyo na kusema uchunguzi zaidi unafanywa. Inadaiwa baada ya kuchafuka kwa bahari, wimbi moja lilipiga sehemu ya mbele ya boti na abiria waliokaa mbele walirushwa na kudondoka baharini.


Awali Ussi aliwataka wamiliki wa vyombo vya baharini vya aina mbali mbali kuchukua kila aina ya tahadhari zaidi katika kipindi hiki ambapo hali ya bahari imechafuka na kuibuka kwa mawimbi makubwa.
Familia mia mbili Wakati huo huo, zaidi ya familia mia mbili hazina makazi ya kuishi baada ya nyumba 24 kuteketea kwa moto huko Shumba mjini katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi alithibitisha kutokea kwa moto huo ambao chanzo chake kinasadikiwa kuwa, watoto walikuwa wakipika chakula.
Dadi alisema nyumba 14 zimeteketea moja kwa moja na moto huo, huku nyingine 10 zikiezuliwa mapaa yake na wananchi kwa ajili ya kuchukua tahadhari ili moto usisababishe madhara zaidi.
Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alifika kuwapa pole wananchi wa kijiji hicho ambao wamepata mkasa wa nyumba zao kuteketea kwa moto.
Alisema kazi inayofanywa kwa sasa na Idara ya Maafa ni kufanya tathmini ya nyumba zote na hasara hiyo kwa ajili ya kutoa fidia ili wananchi warudi katika makazi mapya.

 HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!