Thursday, 2 January 2014

RAIS KIKWETE AMEPOKEA KWA HUZUNI NA MSHITUKO TAARIFA ZA KIFO CHA WAZIRI WA FEDHA WILLIAM MGIMWA.




RAIS Jakaya Kikwete amepokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Kalenga kupitia CCM.
Rais katika taarifa ya Ikulu jana, alisema Taifa limepoteza Waziri huyo katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa, ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Kalenga.



Kifo cha Mgimwa kilitangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali. Katika tangazo lake, Balozi Sefue alisema Waziri Mgimwa aliaga dunia jana saa 5.20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi- Clinic, Pretoria, Afrika Kusini ambako alilazwa kwa muda kidogo.
Balozi Sefue alisema maandalizi ya kurudisha nyumbani mwili wa marehemu yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na taarifa zaidi zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na familia ya Mgimwa, Rais Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshituko na huzuni yangu kubwa kutokana na taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitalini alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Rais Kikwete aliongeza: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu. “Napenda kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wanafamilia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete. Rais pia aliwatumia rambirambi wananchi wa Kalenga akisema wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.
Kifo cha Mgimwa kinafanya wizara tano sasa kukosa mawaziri baada ya wengine wanne kuondoka, kutokana na sakata la ujangili kwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, kukiuka haki za binadamu kwa baadhi ya raia kuuawa na wengine kupata ulemavu huku mifugo pia ikiuawa.
Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alijiuzulu, mawaziri wengine watatu walitenguliwa vyeo vyao, ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Wasifu wake
Mgimwa alizaliwa Kalenga Januari 20, 1950 na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Wasa kati ya mwaka 1961 na 1967 kabla ya kujiunga na Seminari ya Tosa kati ya mwaka 1966 na 1967.
Baada ya hapo alijiunga na Seminari ya Tosamaganga kati ya mwaka 1968 na 1969 kisha Seminari ya Mafinga kati ya mwaka 1970 na 1971.
Mwaka 1975 alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) hadi mwaka 1978 ambapo alipata Stashahada ya Juu katika masuala ya benki.
Alirudi IFM mwaka 1983 na kusoma hadi mwaka 1984 na kutoka na Stashahada ya Uzamili katika fedha na mwaka 1989 alijiunga na Chuo cha Uongozi Mzumbe kusomea Shahada ya Uzamili katika fedha, ambayo aliipata mwaka 1991.
Kuhusu ajira, Mgimwa alifanya kazi Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 2000, akishika nafasi za Mhasibu mwaka 1980 hadi 1981; mwaka 1981 hadi 1989 alikuwa mhadhiri katika Chuo cha NBC na mwaka 1996 hadi 1997 alikuwa Meneja katika benki hiyo.
Kuanzia mwaka 1997 hadi 2000 alikuwa Mkurugenzi wa NBC kabla ya kuwa Mkuu wa Chuo cha Benki Mwanza kati ya mwaka 2000 na 2010, alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kalenga, akichukua nafasi ya Stephen Galinoma.
Mei 7 mwaka juzi aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Fedha, akichukua nafasi ya Mustafa Mkulo.
Ndani ya CCM Mgimwa kati ya mwaka 2008 na 2010 alikuwa Mlezi wa Kata ya Wasa, mwaka 1994 hadi 1995 alikuwa Kamanda Msaidizi wa Vijana wa CCM wakati mwaka 1991 hadi 1994 alipata kuwa Diwani wa Kata ya Gangilonga. Katika uhai wake aliandika machapisho mengi kuhusu masuala ya benki na fedha.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtumia Rais Jakaya Kikwete salaam za rambirambi, kutokana na kifo hicho cha Waziri Mgimwa.
Aidha, kimetuma salaam kwa familia na uongozi wa CCM, kutokana na msiba huo wa kuondokewa na mmoja wa wanachama na mbunge.
Taarifa iliyotolewa jana, ilisema chama hicho kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa za kifo hicho.
“Kwa masikitiko makubwa, CHADEMA kinatuma salaam za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kuondokewa na msaidizi wake wa karibu na mtumishi mwenzake serikalini,” ilisema taarifa ya chama.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!