Thursday, 5 December 2013

WAFANYABIASHARA WAPIGWA RISASI, ARUSHA


Na Joseph Ngilisho, Arusha
MASKINI! Wafanyabiashara wawili, wakazi wa Tengeru, wilayani Arumeru mkoani hapa, Joel Zephania Mzava (35) na Gidiona Kija Mfuru (43), wamenusurika kuuawa baada ya kupigwa risasi na watu wanaodaiwa ni askari wa usalama barabarani.


Mmoja wa majeruhi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Arumeru.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo la kusikitisha lilijiri hivi karibuni kati ya eneo la Msitu wa Mbogo na Karangai wilayani Arumeru, majira ya saa 4:10 asubuhi ambapo wafanyabiashara hao wa kiume walijeruhiwa sehemu mbalimbali.
Gazeti hili liliwakuta watu hao wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Arumeru wakitibiwa majeraha makubwa waliyoyapata.
Mashuhuda hao walisema kuwa, wafanyabiashara hao walikuwa kwenye gari la mizigo aina Nissan Mitsubishi lenye namba T 481 BGF wakitokea wilayani Simanjiro.
Kushoto ni mmoja wa majeruhi baada ya kupatiwa matibabu.
Akizungumza kwa tabu hospitalini hapo, mmoja wa majeruhi hao ambaye amepoteza kipande kwenye sehemu nyeti baada ya kupigwa risasi katikati ya miguu, alisema waliomba lifti katika gari hilo wakitokea Landabani, Simanjiro walikokuwa wamepeleka biashara zao.
Alisema gari hilo lilikuwa na magunia 45 ya mkaa, mali ya dereva wa gari hilo aliyetajwa kwa jina moja la Dismack, mkazi wa Tengeru.
Mzava alisema walipopewa lifti walikaa mbele na dereva hivyo wakawa watatu.
Alisema walipofika eneo la tukio  waliwaona askari wawili wamesimama pembeni ya barabara kwenye kichaka wakiwa na pikipiki aina ya Toyo.
Alisimulia kuwa askari hao waliwasimamisha.
Majeruhi akipatiwa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Arumeru.
Baada ya kusisimama waliwatambua askari hao wanaodaiwa ni wa Kituo cha Mbuguni ambao walimtaka dereva kuwapatia kibali cha kusafirisha mkaa.
Dereva alitoa kibali na risiti za malipo lakini askari hao hawakuridhika na kutaka wapatiwe fedha ndiyo waweze kumwachia vinginevyo wangelipeleke gari kituoni.
Baada ya kuona usumbufu, dereva aliondoa gari ndipo askari mmoja aliwamiminia risasi zaidi ya 20 na kusababisha gari hilo kuserereka na kupinduka huku damu zikiwa chapachapa.
Katika tukio hilo wasamaria wema walifika na kutoa msaada kwa majeruhi kwa kutafuta gari na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi Usa-River ambako walipatiwa hati ya matibabu (PF-3) kisha wakakimbizwa hospitali hiyo ya Wilaya ya Arumeru.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arumeru, OCD Benedict Mapujila alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari ameshapeleke taarifa kwa mkuu wa polisi mkoani hapa, RPC Liberatus Sabas.

GPL

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!