Thursday 12 December 2013

ONGEZEKO LA KURIPOTI VITENDO VYA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA LAFIKIA 14.7% MKOANI ARUSHA.


GEDSC DIGITAL CAMERAMkaguzi wa Jeshi la Polisi toka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoani Arusha Honorina Msoka akitoa zawadi kwa mmoja wa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wodi ya Watoto na akina mama katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru iliyopo mkoani hapa ikiwa ni hatua ya Jeshi hilo kuungana na Wadau wengine duniani kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

GEDSC DIGITAL CAMERAMkuu wa kitengo cha Dawati na Jinsia Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola akimkabidhi moja ya zawadi kwa Msimamizi wa Kituo cha Faraja Bi. Martina Siara ambacho kinahudumia watoto wa mitaani na wanawake waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na mazingira magumu. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)GEDSC DIGITAL CAMERAMkaguzi Msaidizi wa Polisi toka Dawati la Jinsia na Watoto Maria Maswa akiwa anaongea na wanawake waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na mazingira magumu ambao wanalelewa na Kituo cha Faraja kilichopo jijini hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
 Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jumla ya kesi 507 zinazohusiana na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia zimeripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Mkoa wa Arusha ambapoTakwimu hizo ni toka Novemba 2012 hadi Novemba 2013 mwaka huu.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa kitengo hicho Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola wakati watendaji wa ofisi hiyo walipoungana na wadau mbalimbali duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia walipotembelea Shirika lisilo la Kiserikali la Faraja centre linaloshughulika na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na kesi hizo alisema kwamba, idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 14.7 ikilinganishwa na Novemba 2011 hadi Novemba 2012 ambapo kesi 442 ziliripotiwa. Alisema ongezeko hilo linatokana na elimu inayotolewa mara kwa mara na Ofisi hiyo kwa wananchi kupitia mikutano na vyombo vya habari hali iliyowafanya wananchi wahamasike kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa kutoa taarifa katika Ofisi hiyo.
Alisema kati ya kesi hizo, kesi zilizokuwa zinawahusu wanawake ni 280 wakati wanaumeni 120 huku watoto ni 107. Miongoni mwa kesi hizo tayari kesi 132 zimekwishafikishwa mahakamani huku kesi 375 zinaendelea kupelelezwa.
Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto (SSP) Mary Lugola alisema kwamba miongoni mwa kesi zinazoripotiwa katika ofisi hiyo ni pamoja na ubakaji, kulawiti, ukatili dhidi ya mtoto, migogoro katika ndoa na kadhalika.
Akizungumza wakati anawatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo ambao wanalelewa na Shirikalisilo la Kiserikali la Faraja na wagonjwa waliolazwa katika Wodi ya Watoto hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, (SSP) Mary Lugola alisema kwamba katika kuonyesha kujali kitengo cha Dawati kimeamua kuungana nao kwa kuwatembelea na kutoa zawadi mbalimbali kwa makundi hayo.
Kwa upande wake msimamizi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Faraja Young Women Development Organization Bi. Martina Siara alilishukuru jeshi la Polisi mkoani hapa kitengo cha Dawati kwa jinsi linalovyoshirikiana na kituo hicho cha Faraja katika katika suala zima la ulinzi pamoja na utoaji wa elimu na ushauri kwa wanafunzi waliopo kituoni hapo hivyo kuwapa mwanga kuhusiana na haki zao.
Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati Mkoani hapa limeadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa kutembelea kituo cha Faraja na wodi ya watoto katika hospitali ya Mount Meru kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho pamoja na wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo huku likiwa na kauli mbiu ya jeshi hilo nchini isemayo “Zinduka tumia Dawati la Jinsia na Watoto kukemea Ukatili wa Jinsia na Watoto”.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!