Meli ya Maersk Line.
BIASHARA katika bandari ya Dar es Salaam imeanza kushika kasi huku Watanzania wakitarajia kunufaika na punguzo la bei ya bidhaa kutoka nje baada ya meli kubwa yenye urefu wa meta 249 kuanza kutia nanga katika bandari hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa propaganda kuwa bandari hiyo haina uwezo wa meli zenye ukubwa huo wenye kubeba makontena 4,500 kutia nanga, lakini jana Tanzania iliandika historia kwa meli hiyo kutia nanga asubuhi.
Meli hiyo ya Maersk Line ilitia nanga ikiwa inaendeshwa na kapteni wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Abdul Mwingamno ambaye alielezea wazi kuwa hakupata tatizo lolote kutia nanga.
Ikiwa katika safari huonekana hivi.
Kutia nanga kwa meli hiyo kulishuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na kusema kuwa kuanza kutia nanga kwa meli hizo kubwa kutaongeza mizigo kupitia katika bandari hiyo.
“Kwa sasa biashara inazidi kuchanganya kwani nchi za Zimbabwe na Kongo wanapitisha mizigo yao hivyo kwa kutumia meli hizo kubwa gharama zitapungua zaidi ya kuongeza nchi kutumia bandari hiyo,” alisema.
Akizungumzia meli hiyo kutia nanga bandarini, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande alisema kila kitu kinawezekana iwapo kila mtu atafanya juhudi na kuwajibika.
Alisema changamoto watakayokutana nayo sasa ni vifaa vya kupakulia kuendana na ukubwa wa meli ili kuweza kupunguza muda wa kushusha shehena na hivyo kuondoa misongamano bandarini.
Alisema kulikuwa na propaganda ya kuwa meli za ukubwa huo haziwezi kutia nanga katika bandari hiyo hivyo kuishia Mombasa, Kenya na meli ndogo kubeba mizigo mpaka bandarini hapo.
Pia Madeni alizungumzia mgomo wa malori na kusema ulisababisha mlundikano wa mizigo hivyo kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.5 na mpaka jana asubuhi, bado kulikuwa na meli 18 zikisubiri huku tisa zikipakua mzigo.
Alisema wamekuwa katika hatari ya hasara zaidi kwa uchumi kwani idadi kubwa ya mbolea ambazo ni hatari iwapo zingenyeshewa, kwani zilishindwa kusafirishwa.
Naye Meneja mwendeshaji wa kampuni hiyo ya Maersk Line, Amos Mwansumbule alisema meli hiyo iliyotokea katika nchi za Asia na kupitia Afrika Magharibi na kutia nanga Angola, ilisafiri kwa siku 10 kutoka nchini humo hadi Dar es Salaam na ilitarajia kukaa bandarini hapo kwa saa nane
No comments:
Post a Comment