Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu anatajwa kuwa ni Francis Mathias (75), ambaye alikuwa mkazi wa kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru, Joseph Leo, jana alilithibitishia NIPASHE kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa hizo kutoka kwa binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.
“Baada ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango wa chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.
Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania zinazokadiriwa kufikia Shilingi milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000 na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.
Leo alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.
Alipotakiwa na NIPASHE kuthibitisha kama kweli mwananchi wake aliyejinyonga alikuwa raia wa Rwanda, Leo alithibitisha na kufafanua kuwa tayari alikwisha kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika opereshani iliyoanza Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.













No comments:
Post a Comment