Wanasayansi kutoka chuo
kikuu cha tiba Washington, Marekani wamegundua katika utafiti wao kuwa sumu
iliyopo katika mwili wa nyuki iitwayo toxin melittin inaweza kuvivunjavunja na
kuviharibu virusi vya Ukimwi pasipo kuacha madhara katika chembehai za
mwili. Habari
hii imeelezwa katika taarifa ya tiba za dawa za kupunguza makali ya virusi vya
Ukimwi iliyotolewa mapema mwaka huu.
Watafiti
hawa wanaeleza kuwa matokeo ya utafiti huu kufika katika hatua kubwa inayoleta
matumaini ya kupamba na VVU kwa kuweza kupata dawa ya kupaka ya majimaji ndani
ya uke itakayotumika kupambana na maambukizi ya VVU.
Dk Joshua Hood anasema:
“Matumaini yetu ni kwa maeneo ambayo hali ya maambukizi yapo juu na vigumu
kuzuilika, dawa ya majimaji mazito inaweza kutumika kupaka ndani ya uke katika
kuzuia maambukizi ya mwanzoni kabisa.”
Sumu ya nyuki, melittin,
imeonyesha uwezo wa kupambana na VVU kwa kuvunja ganda linalomzunguka kirusi na
virusi wengine kwa kulitoboa na kuacha matundu.
Mwandishi mwandamizi wa
makala za biokemia, Dk Samuel Wicline, Profesa wa Biochemia wa Taasisi ya
Russel Hornsby anafafanua kuwa kuwa vijipande vidogo vilivyoshindiliwa vya sumu
ya nyuki vimeonyesha kuwa na tabia ya kuweza kuua chembe hai zenye
saratani.
Anaeleza mtaalamu huyo kuwa
hii si mara ya kwanza katika ugunduzi wa tiba ya namna hii, kwani mwaka 2004
wanasayansi wa Croatia walitoa taarifa yao katika jarida la sayansi ya chakula
na kilimo kuwa mazao ya nyuki, ikiwamo asali na sumu ya nyuki vina uwezo wa
kutumika kutibu na kuzuia saratani.
Chembehai za mwilini zenye
afya huendelea kubaki salama pasipo kupata madhara wakati wa tiba kwani sumu
hiyo ya nyuki imetengenezewa na kitu kama ngao ambayo ikikutana na seli za mwili
hudunda na kwenda mbali bila kujishikiza.
Hii ni kwa sababu ya seli
za mwili ni kubwa kimaumbille kuliko sumu ya melittin, wakati kwa virusi vya
Ukimwi ni vidogo kuliko melittin, hivyo ikikutana navyo ngao hiyo haiwezi kuzuia
kirusi kidunde kwani ni kidogo, hivyo kirusi hudakwa na melittin na
kushikamana, hivyo kirusi huweza kuharibiwa.
Dk Hood anaeleza kuwa
vijipande vilivyoshibishwa na sumu ya melittin huweza kushikamana na kirusi na
kutoboa tundu katika ganda la kirusi na kuchana ganda lote, hivyo kirusi huweza
kuvunjwa.
Wakati tiba kwa kutumia
dawa za kufubaza makali ya VVU, yaani ARVs zinafanya kazi kwa kuzuia uwezo wa
virusi kujidurufisha, kwa tiba ya melittin hushambulia sehemu muhimu ya
kimaumbile ya virusi ambayo ndiyo nguzo imara kwa virusi.
Tatizo katika tiba ya
kuzuia uwezo wa kirusi kujidurufisha ni kuwa maambukizi yanakuwapo na hayakomi
mwilini, hivyo hayazuii maambukizi kuwepo mwilini.
Baadhi ya vipande vya
virusi vya Ukimwi vimepata uwezo wa kujibadili hivyo kuzuia ufanyaji kazi wa
ARVs na hivyo kuendelea kuzaliana na kuvamia seli za mwili.
Mtaalamu huyo anaeleza:
“Tunashambulia sehemu ya kimaumbile ya kiurithi ya VVU, kinadharia, tunasema
hakuna namna yoyote ya kirusi kuweza kujibadili ili kukabiliana na mazingira
mapya ya kujihami na mashambulizi ya tiba hii ukilinganisha na mashambulizi ya
ARVs’ kirusi kitahitaji kuwa na ganda la kujikinga lenye ngozi ya tando mbili
ili kuweza kujibadilisha.
Dk Hood anaamini kuwa sumu
ya nyuki iliyoshibishwa vijipande vya melittin ina uwezo wa kitiba wa aina mbili
katika kutibu na kuzuia, moja ikiwa kutumika kama maji mazito ya kuweka ukeni
(vaginal jelly) ili kuzuia maambukizi ya VVU kuenea .
Tiba ya pili ni kutumika
kwa maambukizi ambayo tayari yapo mwilini hasa kwa maambukizi yaliyoleta usugu
wa dawa, kinadharia ni kuwa kama sumu ya melittin itadungwa mwilini na kuingia
katika mzunguko wa damu inaweza kuviangamiza virusi vya
Ukimwi.
Anaeleza Dk Hood kuwa,
“Kimsingi, vijipande hivi vya tiba vilivyotumika vilianza kufanyiwa majaribio ya
kimaabara miaka mingi iiliyopita ikiwa kama zao la damu bandia ya kutengenezwa
maabara.
Hata hivyo, haikufanya
vyema katika kubeba na kusambaza hewa ya oksijeni, lakini ikawa ikizunguka
katika mzunguko wa damu ikiwa salama mwilini na hivyo ilitupa mwanga wa kuweza
kupata mbinu mpya ya kupambana na maambukizi ya aina
tofauti.”
Melittin inashambulia tando
mbili za ngozi laini pasipo kutofautiana, hii inaifanya melittin iwe dawa yenye
uwezo wa juu kitiba katika mapambano dhidi ya maambukizi VVU.
Virusi kama Hepatitis B
(homa ya ini) na C ambavyo navyo vina ganda la kuwakinga la namna hii navyo
vinakuwa miongoni mwa virusi vinavyoweza kuangamizwa na tiba ya
melittin.
Pia, majimaji mazito
(jelly) ya melittin pia huenda yakalenga mbegu za kiume. Mtafiti Hood anaeleza
kuwa inaweza kutumika kama dawa za kuzuia mimba, hivyo kuwa kama njia ya uzazi
wa mpango. Hata hivyo, bado hawajalifanyia kazi.
Pia, wanaangalia uwezekano
wa wenza wawili ambao mmoja wao aliyeambukizwa VVU pale watakapohitaji kupata
mtoto aliye salama, kwani vijipande hivyo vya melittin ni salama kwa mbegu za
kiume kwa sababu hiyohiyo ni salama pia kwa seli za ukeni.
Dk Hood anasema bado ni
mapema mno kwani mpaka sasa majaribio yote ni ya kimazingira ya
kimaabara.
Kwa namna yoyote
itakavyokuwa, vijipande hivi vya melittin ni rahisi kuvitengeneza vya kutosha na
itakuwa rahisi kuvisambaza kwa ajili ya majaribio ya baadaye kwa
binadamu.
Hata hivyo, hiyo itakuwa ni
habari njema endapo utafiti huo utafanikiwa na kuleta matokeo mazuri katika vita
dhidi ya VVU, pia itakuja kuwa na faida kiuchumi kwa wafugaji wa nyuki nchini
wakiwamo wa Tanzania.
Habari na Samwel Shita,
Mwananchi
Chanzo -
Mwananchi
No comments:
Post a Comment