KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji na kata ya Mkwajuni Wilaya ya
Chunya Mkoani hapa wamemzika Mwanakijiji mwenzao akiwa hai wakimtuhumu
kusababisha kifo cha Mkazi mmoja kijijini hapo.
Tukio
hilo la kusikitisha limetokea Apri 26 mwaka huu majira ya Saa Nane Mchana
katika Kitongoji cha Maweni Makaburini baada ya Mhanga aliyefahamika kwa jina la
Victory Mwachirui(68) kuhudhuria mazishi ya Pita Barton(28)aliyefariki baada ya
kuugua kwa muda mrefu.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Thobias Ismail amesema marehemu alipatwa na
umauti akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga wa jadi ambaye jina lake halikuweza
kujulikana maramoja.
Amesema
wakati taratibu za mazishi zikiendelea Ndugu wa marehemu walidai kuwa kifo cha
Marehemu kilisababishwa na Mwachirui ambaye ni Katekista mstaafu kwa imani za
kishirikina.
Ameongeza
kuwa wakati kaburi likichimbwa kwa ajili ya kumzika marehemu ndipo vijana
waliokuwa wakichimba waliagiza Wazee wa Mila wafike makaburini kwa ajili ya
kuangalia utaratibu wa mazishi na kukagua ukubwa wa Kaburi ambalo lilikuwa
limekwisha chimbwa.
Kutokana
na mwito huo walifika wazee wanne akiwemo Mzee Mwachirui ambaye walimsisitiza
kusogea jirani na kaburi ambapo baada ya kusogea alipigwa na Sururu kichwani na
kuangukia kaburini huku akisindikizwa na marungu.
Baada
ya Mzee huyo kupoteza fahamu Vijana hao walianza kutandika fito ndani ya kaburi
kisha kufukia kwa udongo kiasi kwa lengo la kutenganisha na Mwili wa Marehemu
Pita uliokuwa kwenye jeneza baada ya kuwazika kwenye kaburi
moja.
Baada
ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi la vijana lilielekea hadi nyumbani kwa
Mzee aliyezikwa akiwa hai na kuiteketeza nyumba yake huku wakiapa kutotoa siri
wakidai Siri ya Jeshi.
Jeshi
la Polisi baada ya kufanya upelelezi na kubaini kitendo hicho waliwaamuru baadhi
ya Vijana kufukua kaburi hilo zoezi ambalo lilifanyika baada ya Vijana hao
kulipwa.
Baada
ya kufukuliwa kwa kaburi hilo Mwili wa Marehemu Mzee Mwachirui ulichukuliwa na
kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Mkwajuni kwa ajili ya Uchunguzi huku
Mwili wa Pita ukizikwa upya palepale.
Baada
ya kukamilika kwa uchunguzi mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili
ya mazishi ambapo Marehemu alizikwa katika eneo tofauti na alipokuwa amefukiwa
awali.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
ambapo pia ametoa wito na kuwaasa wananchi na jamii kuacha tabia ya kuamini
mambo ya ushirikina na uchawi kwa madai kuwa hauna faida kwao bali huchochea
migogoro katika jamii zao.
Aidha
ameongeza kuwa wakumbuke kitendo cha kujichukulia sheria mkononi ni kosa
kisheria ambapo pia amewaomba wenye taarifa za walipo waliohusika na mauaji
hayo kuzifikisha polisi haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao
ingawa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.
Picha
na E. Kamanga wa Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment