Monday 6 August 2018

Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isack Sepetu amemuhuku Mfanyabiashara Abdallah Mohamed Kangoba adhabu ya kunyongwa hadi kufa

MUNIR ZACHARIA

Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isack Sepetu amemuhuku Mfanyabiashara Abdallah Mohamed Kangoba mwenye umri wa miaka 43, adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe kwa kumpiga mapanga baada ya kunyimwa tendo la ndoa usiku wa kuamkia Oktoba 3, mwaka 2013 katika kijiji cha Donge Mtambile, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Jaji Mkusa Isack Sepetu ametoa uamuzi huo, baada ya upande wa mashitaka kukamilisha kutoa ushahidi ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali Mohamed Saleh na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Msomi Rajab Abdallah na kuridhika kuwa mshitakiwa ametenda kosa la mauaji kwa kukusudia.
Akisoma hukumu hiyo kwa muda wa saa moja na kupitia vielelezo vya ushahidi uliotolewa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Polisi Mkokotoni na Daktari dhamana aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, Jaji Mkusa amesema ameamua kutumia kifungu cha 196 na 197 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004, ya mwenendo wa makosa ya jinai kutoa adhabu ya kifo kwa mshitakiwa.
Jaji Mkusa amesema kulingana na ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama, mshitakiwa amemuua mkewe, kwa kukusudia baada ya kumpiga kwa mapanga kichwani wakati alipokuwa akiswali Sala ya Alfajiri akiwa katika Tahiyatu, muda mfupi baada ye kurejea kutoka Msikitini na kufanya tendo hilo kabvla ya kwenda kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza baada ya Mahakama kumtia hatiani, Wakili wa Mshitakiwa Rajab Abdallah amesema Mahakama inapaswa kutoa adhabu yenye unafuu kwa sababu mshitakiwa bado ni mtu mwenye umri wa kuweza kuchangia nguvu kazi ya taifa na hana kumbukumbu ya kufanya makosa kama hayo katika maisha yake.
Akijitetea baada ya kupewa nafasi na Jaji Mkusa Isack Sepetu, mshitakiwa Abdallah Mohamed Kangoba ameiomba Mahakama Kuu ya Zanzibar kumpa adhabu nafuu, na kueleza kwamba amewahi kuoa wake wanne na wote ameachana nao katika mazingira ya amani na kueleza kadhia hiyo ya kumuua mkewe yeye hahusiki kinyume na maelezo aliyoyatoa baada ya kuripotia Polisi siku ya tukio.
Kwa mujibu wa maelezo ya ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo, Marehemu na Mumewe wamekubaliana kufanya tendo la ndoa siku moja na kupumzika siku ya pili yake, jambo ambalo Mumewe usiku wa kuamkia Oktoba 3, mwaka 2013 amevunja makubaliano na kutaka kulazimisha kupatiwa tendo la ndoa kinyume na maafikiano yao, na kuchukua uamuzi wa kumpiga kwa mapanga huku akiwa na ujauzito wa miezi miwili na nusu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!