Sunday 6 May 2018

Marekani yatoa tril 1.2 kukabili VVU, ukimwi

SERIKALI ya Marekani kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), umeahidi fedha zaidi Dola za Marekani milioni 512 (takribani Sh trilioni 1.17) kupambana na janga la VVU/Ukimwi nchini Tanzania.


Habari hizo njema zimetangazwa jana Dar es Salaam na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inmi Patterson wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam akiwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile. Ukiwa umeandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, Mpango wa PEPFAR nchini unalenga kudhibiti janga la Virusi vya Ukimwi - VVU/ Ukimwi ifikapo Septemba 2019. Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR, imetumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 4.5 (takribani Sh trilioni 10.26) kuzuia maambukizi ya VVU/Ukimwi nchini tangu 2004.
“Ninayo furaha kutangaza leo kwamba kupitia PEPFAR, Serikali ya Marekani itatumia fedha zaidi Dola milioni 512 (takribani Shilingi trilioni 1.17) kuboresha kinga ya VVU, upimaji na tiba nchini Tanzania hadi Septemba 2019. “Matokeo kutoka Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi Tanzania ya Desemba 2017 yametuonesha kwamba Tanzania iko nyuma ya nchi nyingine za kikanda. Mathalan, ni karibu nusu tu ya waathirika wa VVU nchini waliopimwa na kujua kwamba wana VVU. Tanzania inabidi irudi katika mstari na hii itahitaji juhudi kubwa katika uelimishaji umma na watu kupimwa, juhudi za haraka kuendana na sera mpya, na utekelezaji wa haraka wa sera hizo,” alisema.
PEPFAR inahamasisha kila mtu, hususan wanaume, kuongea na wafanyakazi wa afya kuhusu kupimwa VVU. Mtu yeyote anayegundulika kuathirika na VVU anaweza kuanza matibabu mara moja. Takribani Watanzania milioni moja walioathirika na VVU wako katika tiba ya kuokoa maisha, na wengi wao wanaishi maisha marefu na ya afya na wana viwango vya chini vya virusi kiasi kwamba hawawezi kuwaambukiza wengine, wakiwemo wenza wao na watoto.
Kuhusu Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) nchini Tanzania, katika mwaka wa fedha 2017 pekee, PEPFAR ilipima VVU kwa Watanzania milioni tisa, inahudumia Watanzania 950,000 walio katika tiba ya kuokoa maisha yao. Lengo ni Watanzania milioni moja kuwa katika tiba ya kuokoa maisha yao ifikapo mwisho wa 2018. Katika mwaka wa fedha 2017, PEPFAR ilitoa tiba ya kuokoa maisha kwa wajawazito 56,000 ili kuzuia maambukizi ya VVU kati ya mama na mtoto.






No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!