Tuesday, 24 April 2018

Ugonjwa wa kisukari tishio

SERIKALI imekiri kuwa ugonjwa wa kisukari, unazidi kuwa tishio nchini na kuhamasisha watanzania kuzingatia misingi ya lishe bora, kufanya mazoezi na kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara.


Hayo yalibainishwa bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Dk Christine Ishengoma (CCM).
Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua serikali, ina mpango gani wa kufanya utafiti kuhusu dawa za kisukari, kwa kuwa hadi sasa hakuna dawa sahihi za kutibu ugonjwa huo.
Akijibu swali hilo, Dk Ndungulile alisema ugonjwa wa kisukari ni moja ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza, ambayo kwa sasa kutokana na mtindo wa maisha, unazidi kuenea kwa kasi nchini.
"Ugonjwa huu husababishwa na kichochezi kiitwacho Insulin, aidha kwa kushindwa kutengenezwa kabisa kwa kongosho au kufanyakazi chini ya kiwango," alieleza. Alisema kwa sasa asilimia 13 ya watanzania, wanaugua ugonjwa wa kisukari.
"Natoa rai magonjwa kama haya yasiyoambukiza huchangiwa sana na tatizo la lishe duni, matumizi ya sigara, kutokufanya mazoezi na pombe kupita kiasi. Naimba watanzania tuanze kuchukua hatua kuepuka kulinda afya zetu," alisema.
Dk Ndungulile alikiri kuwa dawa ya kutibu ugonjwa huo, haijagundulika duniani mpaka sasa. Kwamba ili kupona, mgonjwa anatakiwa kuhakikisha kiwango chake cha sukari mwilini, kinakuwa ndani ya kiwango cha kawaida kila siku.
Alisema pia tiba nyingine ni dawa aina ya sindano ya Insulin, ambayo mgonjwa huchomwa kila siku kwa maisha yake yote na vidonge anavyotakiwa kumeza kila siku.
Alisema kwa kutambua ongezeko la wagonjwa wa kisukari nchini, serikali katika bajeti yake ya 2018/19 imetanga Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya kununulia dawa hiyo aina ya Insulin.
Hata hivyo, alisema kuna tafiti nyingi zinaendelea duniani kote ili kutafuta dawa itakayoweza kutibu ugonjwa huo, lakini tafiti hizo bado hazijazaa matunda.
"Tafiti hizi ni pamoja na zile za kujaribu kutengeneza seli za kongosho na kuzipandikiza ili kuweza kuweka seli mpya za kongosho na kuipa kongosho uwezo wa kutengeneza insulin kwa wingi zaidi,"alisema.
Alisema njia hiyo pekee, ndio itakuwa ufunguzi wa kudumu wa tiba dhidi ya ugonjwa huo. Mara tafiti hizo zitakapokamilika na kuonesha mafanikio, serikali ya Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana hapa nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!