Wednesday 18 April 2018

Safari za ATCL anga za Ulaya, Asia zanukia

MALENGO ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ya kutaka kufanya safari za bara la Ulaya, Asia na Marekani, yako mbioni kutimia kutokana na ujio wa ndege ya kisasa aina ya 787 Dreamliner, inayotarajiwa kuwasili Julai mwaka huu.


Hatua hiyo itafanya shirika hilo la ndege kutoa huduma ipasavyo katika sekta ya anga na kukamata soko kwenye nchi za Afrika Mashariki, ambalo kwa sasa imeshikiliwa na nchi za Ethiopia, Kenya na Rwanda.
Makamu wa Rais wa Mauzo katika Kampuni ya Ndege ya Latin Amerika, Afrika na Visiwa vya Caribbean, Van Rex Gallard alithitisha kuwa Tanzania imetoa oda ya ndege moja ya 787-8 Dreamliner, yenye thamani ya dola za Marekani milioni 224.6 na itaendeshwa na ATCL.
Hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema wanatarajia kuanza Safari za Ulaya, Asia na Marekani katika kipindi kifupi na ndege hizo ni imara kufikia lengo hilo.
Alisema Tanzania ilitia saini makubaliano na kampuni ya Bombardier Commercial Aircraft ya kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 Julai mwaka 2016 na miezi mitano baadaye walisaini kununua Boeing 787-8 Dreamliner. Matindi alisema Bombardier C300s, zitatumia kufungua safari za usafiri wa anga katika kanda sita za Kusini na Magharibi mwa Afrika, kwa lengo la kupata masoko hayo.
“Tuna lengo la kukamata masoko ya Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe na baadaye kufika nchi za Afrika Magharibi za Ghana na Nigeria pamoja na kutumia ndege ya Dreamliner katika safari za kimataifa za China na India na baadaye kufuatiwa na kwenda bara za Ulaya katika awamu ya pili,” alisema.
ATCL inatarajia kupata cheti kutoka taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa usalama na viwango kwa mashirika ya ndege duniani IOSA, kabla ya Juni mwaka huu, hali itakayowezesha kushirikiana kibiashara na watoa huduma wengine ili kuongeza mapato kupitia makubaliano ya hisa.
Miaka miwili iliyopita, Tanzania ilianza mkakati wa kufufua shirika hilo la ndege la serikali kwa kuweka mikakati mbalimbali.
Katika programu hiyo waliweka mikakati ya kununua ndege mpya sita kati ya mwaka 2016 hadi 2018, kulipa madeni na kuongeza mtaji na kukuza na kuendesha biashara kwa njia za kisasa.
Kwa sasa, licha ya kuanza kusaka ofisi katika nchi mbalimbali, ATCL imetangaza ajira mpya 88 zikiwemo za wahudumu katika ndege.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!