Tuesday, 6 March 2018

Tanzania yasikitishwa na kauli za Magharibi

MABALOZI wa kigeni wanaofanya kazi nchini Tanzania wametakiwa kutambua mazingira changamani yanayokabili Taifa hili kabla ya kutoa ripoti kwa umma ambazo hawajathibitisha zenye kuchochea mhemko.

Kauli hiyo imo katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga (pichani) kwa vyombo vya habari jana. “Kwa upande wetu, tunakaribisha mazungumzo yenye uwazi kati yetu na marafiki na washirika wetu katika masuala mbalimbali yanayohitaji ufafanuzi ili wawe na taarifa sahihi za mambo yanayotukia,” alisema Dk Mahiga.
Aidha katika taarifa yake aliongeza; “Vyombo vya dola vimeendelea na shughuli yake ngumu ya kuchunguza matukio yaliyotokea hivi karibuni yenye viashiria vinavyotishia usalama na uhusiano wake na masuala ya kisiasa. Busara ya kawaida inatutaka kuruhusu sheria kuchukua mkondo kwa kuwa na subira.” Taarifa imetolewa siku chache baada ya balozi za Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na baadhi ya mataifa ya Magharibi kuelezea shaka kwa matukio ya kiusalama yaliyotokea hivi karibuni.
Katika taarifa zao mataifa hayo yamesema kwamba matukio hayo ni tishio kwa demokrasia na utawala bora. Kuhusiana na suala la usalama nchini, Balozi Mahiga alisema kwamba taarifa zilizotolewa na nchi hizo zinaonesha kutojua changamoto za kiusalama na kisiasa zinazokabili taifa hili katika kipindi cha miezi 18 iliyopita. “Mbaya zaidi taarifa zao zimetolewa bila kujua hali ya kisiasa na usalama nchini,” alisema.
Dk Mahiga ambaye alishawahi kutumikia nafasi ya kuwa balozi wa kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, alisema kwamba ni kawaida kwa mbalozi wa kigeni kufuatilia masuala ya kisiasa na kiusalama katika nchi walizopo na kupeleka taarifa katika nchi zao. “Hata hivyo tulifadhaishwa na ukimya uliojitokeza kwa mabalozi hao wakati kukiwa na changamoto ya matatizo ya kiusalama katika maeneo ya Kibiti-Mkuranga- Rufiji.
“Watu kadhaa walikufa katika mazingira ya kutatanisha na wengi wao kutoka chama tawala,” alisema Waziri katika taarifa yake. Dk Mahiga alisema kwamba mauaji katika eneo hilo yalifanywa baada ya kuwapo kwa vitendo viovu vilivyokuwa vinatokea maeneo mbalimbali ya nchi. “Pamoja na kelele nyingi kupigwa na vyombo vya habari vya hapa nchini hakuna hata neno moja lililotolewa na mabalozi na wawakilishi hao kulaani hali hiyo. “Ni leo Umoja wa Ulaya unatoa taarifa kuhusu tukio lililofanyika mkoa wa Pwani miaka miwili iliyopita. Rejea hii ya sasa hakika inatia shaka,” alisema.
Waziri alisema kwamba mabaki ya watu waliokuwa wakihusika na uhalifu huo wanaendelea kufanya maovu katika juhudi za kufuta alama zao ili wasikamatwe. Alisema moja ya taarifa zilizotolewa na mabalozi hao, zimetambua wito wa Rais John Magufuli wa kuchunguza vurugu nyingine kabla ya mashambulio ya Kibiti- Mkuranga-Rufiji. “Hata hivyo taarifa hiyo imeshindwa kutambua uhusiano uliopo kati ya maamuzi magumu ya Rais Magufuli ya kukabiliana na rushwa, dawa za kulevya, wakwepaji kodi, ujangili na kurejesha uwajibikaji katika sekta ya umma na binafsi na masuala haya ya usalama,” alisema.
Dk Mahiga alisema anaamini kwamba hatua zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya tano za kukabiliana na hali hiyo zimeibua elementi zilizokuwa zinachezea nchi kutokana na udhaifu uliokuwapo awali. “Watu hawa wanapambana na mabadiliko yanayoletwa kwa kutengeneza maovu kwa lengo la kuipaka matope serikali kupitia mgongo wa siasa,” taarifa ilisema. Hata hivyo, Dk Mahiga alisema kwamba serikali ya Tanzania itaendelea na juhudi zake za kuwa la amani kama historia yake inavyosema ikiheshimu utawala wa sheria na kuthamini demokrasia.


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!